"Maisha yangu yamo hatarini!" Ex wa Eric Omondi adai baada ya kudhulumiwa na mpenzi wake

Muhtasari

•Chantal amedai kuwa baada ya kuingia kwake, mpenzi huyo wake alimpiga kwa hasira na kumsukuma  kwenye ngazi.

•Chantal anadai kuwa maisha yake yamo hatarani huku akileza kuwa Nicola alitishia kurudi baadae na kuendelea kumpiga.

Nicola, Chantal na Eric Omondi
Nicola, Chantal na Eric Omondi
Image: INSTAGRAM

Chantal Grazioli hatimaye amesimulia matukio yaliyojiri Ijumaa asubuhi ambapo inadaiwa alishambuliwa na mpenzi wake Nicola Traldi.

Kipusa huyo mwenye asili ya Italia ameeleza kuwa Nicola ambaye alikuwa mlevi wakati huo alivunja mlango wa nyumba yake baada ya kukataa kumfungulia..

Chantal amedai kuwa baada ya kuingia, mpenzi huyo wake alimpiga kwa hasira na kumsukuma  kwenye ngazi. Aidha amefichua kuwa mpenziwe amekuwa akimdhulumu mara kwa mara.

"Mara nyingi ameniagiza nijiepushe na vyombo vya habari, jambo ambalo nilifanya kwa kuhofia kudhalilishwa na kushambuliwa. Niliogopa kujitokeza lakini siku ya Ijumaa ikiwa mbaya zaidi, nilijaribu kumfikia mama yangu bila mafanikio, wakati huo huo majirani zangu, walinzi na caretakeri walikuja kuniokoa," Chantal alisimulia kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Chantal alieleza kuwa baada ya kusaidiwa na majirani alichukua hatua ya kumpigia mpenziwe wa zamani Eric Omondi kwa ajili ya usaidizi zaidi.

Mchekeshaji huyo alimsaidia kutafuta matibabu zaidi hospitalini na kupiga ripoti katika kituo cha polisi.

"Tulifuata itifaki zote ambazo zilitakiwa kutoka kwetu na polisi na hospitali (za kibinafsi na za umma) lakini mpaka sasa Nicola hajakamatwa na alichukua sim kadi yangu, simu yangu, funguo za gari na funguo za nyumba yangu," Alisema.

Malkia huyo sasa anadai kuwa maisha yake yamo hatarani huku akileza kuwa Nicola alitishia kurudi baadae na kuendelea kumpiga.

"Hii inaweka maisha yangu hatarini kwani sijui atafanya nini baadaye. Iwapo anadai kuwa anasingiziwa kwa nini asijipeleke kwenye kituo cha polisi? Hapatikani ata," Aliongeza.

Chantal amelaani vikali unyanyasaji wa kijinsia huku akitoa wito kwa suala hilo kuangaziwa zaidi hapa nchini.

Baada ya Eric Omondi kuchapisha taarifa ya kushambuliwa kwa mpenzi huyo wake wa zamani, Bw Nicola alitumia ukurasa wake kufutilia mbali madai hayo na kusisitiza kuwa hana hatia.

"Nimesingiziwa kwa jambo ambalo singefanya kamwe, lisilosemeka, Ni siku ya huzuni.. Nisingewekelea mikono yangu juu ya mwanamke. Mimi ni baba wa mabinti wawili. Ukweli utajulikana," Aliandika.

Aidha mjasiriamali huyo alibainisha kuwa mama yake alimfunza maadili mema na hata watu wa karibu naye wanafahamu hawezi kupiga mwanamke.