"Nitaacha urithi bora bila watoto!' Mjukuu wa Kibaki afichua sababu hataki watoto

Muhtasari

•Mwanamitindo huyo alibainisha kuwa angependelea kuitwa mjomba badala ya kuwa na watoto wake mwenyewe.

•Aliweka wazi kuwa kwa sasa hayupo kwenye mahusiano yote na hayupo makini kutafuta mpenzi.

Image: INSTAGRAM// SEAN ANDREW

Mjukuu wa rais wa tatu wa Kenya Mwai Kibaki, Sean Andrew amesisitiza kuwa hataki kuwahi kupata watoto.

Mwaka jana Andrew aliwashangaza wengi baada ya kudai kuwa hajawahi kupatwa na wazo la kuwa baba.

“Ndio nimewahi fikiria kuoa na kutulia katika ndoa lakini hata siku moja sijawahi jifikiria au kujiona kuwa baba. Pengine niwe mume tu lakini sitaki watoto,” Alisema katika kipindi cha Q&A kwenye Instagram.

Katika mahojiano ya hivi majuzi, Andrew aliweka wazi kuwa ni angepelea kuwafuga wanyama kipenzi wanyama kuliko watoto.

Aidha, mwanamitindo huyo alibainisha kuwa angependelea kuitwa mjomba badala ya kuwa na watoto wake mwenyewe.

"Sijui, ni wazo ambalo lilinikujia kwa muda mrefu. Watoto hawajakuwa mojawapo ya ajenda zangu. Nadhani nitaacha urithi bora bila watoto," Andrew alisema katika mahojiano na Mpasho.

Ingawa hataki kupata wake mwenyewe, Andrew aliweka wazi kuwa hana chuki yoyote dhidi ya watoto.

"Watoto ni wazuri lakini sijawahi kujiona kama baba," Alisema.

Mtoto huyo wa mfanyibiashara Jimi Kibaki hata hivyo hakutupilia mbali suala la kuwahi kujitosa kwenye ndoa.

"Ikitokea ningependa kuwa kwenye ndoa, ningependa kushiriki maisha yangu na mtu. Lakini sitazamii hilo," Alisema.

Andrew alifichua kuwa hapo awali amewahi kuwa kwenye mahusiano kadhaa lakini hakuna ambayo yalifua dafu.

Aliweka wazi kuwa kwa sasa hayupo kwenye mahusiano yote na hayupo makini kutafuta mpenzi.