(Videos) Mtangazaji amfanyia mbwa wake aliyekufa mazishi ya kifahari

Akiulizwa kwa nini alitumia pesa nyingi kufanya mazishi ya mbwa, ndiki alisema alimpenda sana mbwqa wake.

Muhtasari

• Mtangazaji huyo aliwakashfu watu waliokemea kitendo chake kutumia pesa nyingi kwa ajili ya mazishi ya mbwa.

• Alisema yeye ndiye aliyejua jinsi mbwa huyo alikuwa wa maana kwake na watu waache kupangia watu mambo yao.

Mtangazaji mmoja kutoka nchini Afrika Kusini amegonga vichwa vya habari kote ulimwenguni baada ya kuandaa mazishi ya haiba ya juu kwa ajili ya mbwa wake aliyefariki.

Moshe Ndiki ambaye ni mtangazaji wa redio na runinga alipakia video kwenye ukurasa wake wa Instagram akionesha maandalizi kabambe yenye haiba ya juu kwa ajili ya kumuaga buriani mbwa wake Sugar Ndiki ambaye alikufa juzi kati.

“Nimekuwa nikipitia wakati mgumu zaidi ya siku mbili zilizopita, nikijaribu kuiweka kando ili tu nifanye kazi na kujiambia nitahuzunika Jumapili. Baby, nakupenda sana @sugarndiki. Ninakupenda na natumai upande wa pili utakutendea vyema. Nimefurahi kukupenda, kukufahamu, na kuwa baba na mama yako.” Aliomboleza mtangazaji huyo.

Ndiki alielezea kumbukumbu za uhusiano wake na marehemu mbwa wake huku akisema kwamba yeye ndiye alikuwa kifungua mimba wake na Rafiki mkubwa.

“Kumbukumbu nyingi sana, umekuwa mzaliwa wangu wa kwanza, na ni huruma gani haukuweza kukutana na ndugu yako. Nimevunjika moyo na ninajiuliza nitakuwa nini bila wewe Sugar. Nakupenda sana lwam. Mazishi na mipango ifaayo itafanywa hivi karibuni,” Moshe aliongeza.

Katika mazishi hayo ambayo yaliandaliwa na kundi kwa jina NONO Events ambapo uvaaji wote ulikuwa wa nguo na kila kitu cheupe kama theluji, Ndiki aliwashukuru wote waliojumuika na yeye katika kutuma risala za rambirambi kwa kumpoteza mbwa wake mpenda.

“Asante kwa kila mtu aliyetuma salamu za rambirambi, kuhudhuria mazishi na kututumia ujumbe wa kuchangamsha moyo, umethaminiwa sana, asante kwa marafiki na familia yangu kwa kuelewa maumivu yangu na jinsi nilivyompenda mtoto wangu, @sugarndiki daima na milele,” aliandika kwenye Instagram Ndiki.

Katika mahojiano alipoulizwa ni kwa nini aliamua kufanya mazishi ya kifahari kwa mbwa wake hivyo, Ndiki alisema kwamba alikuwa ameishi na mbwa huyo kwa muda wa miaka mitano na kumfanyia heshima ya mazishi kama hiyo hakuona hasara kwa sababu watu pia hufanyiqa wapendwa wao hivyo wanavyoaga dunia. Pia alisema tu kwamba alijua watu watasema mambo mengi eti ni kwa nini hakutumia pesa hizo kusaidia binadamu lakini ndio hivo alishaamua kumpa buriani ya heshima mbwa wake.

“Watu ni watu na ni katika asili yao kuzungumza na kuguswa na mambo ambayo hawayafahamu. Sijawahi kwenda kwenye mazishi ya mbwa, ilikuwa mara yangu ya kwanza kuhudhuria na kuandaa. Lakini si kuhusu wakosoaji. Watu wanapenda kuweka kiwango fulani cha kutumia viwango vyao wenyewe,” alisema Ndiki.