"Mimi ni tajiri wa mbegu!" Mbosso ajigamba kuhusu kuwa na watoto wengi

Muhtasari

•Mbosso  ameonekana kumpendelea zaidi  aliyekuwa mpenzi wake Rukia, na ambaye ni mama ya mwanawe Ikram. 

•Alisema kuwa mtoto wake na Bi. Rukia ni, "Mwanangu wa dhahabu."

Image: INSTAGRAM// MBOSSO

Staa wa Bongo Mbwana Yusuf Kilungi almaarufu Mbosso ni miongoni mwa wasanii wanaofahamika kuwa na watoto wengi  na wanawake tofauti.

Kufikia sasa, kundi kubwa la wanawake wamewahi kujitokeza kudai kuwa na mtoto pamoja na msanii huyo wa WCB.

Akiwa kwenye mahojiano ya kipekee na Wasafi Media, mwanamuziki alieleza kuwa amebarikiwa na uwezo wa kupata watoto wengi.

"Mimi ni tajiri wa mbegu. Maumbile tu, Mungu kaniumba hivo. Niko nacho," Mbosso alisema.

Staa huyo alikuwa anajibu kuhusiana na suala la wanawake wengi kujitokeza kudai kuwa yeye ni mzazi mwenzao.

Ingawa idadi halisi ya wanawake ambao amewahi kupata watoto nao haijulikani, Mbosso kwa kawaida huwa hafichi ukweli kuwa yeye ni baba wa watoto wengi.

Mbosso hata hivyo ameonekana kumpendelea zaidi  aliyekuwa mpenzi wake Rukia, na ambaye ni mama ya mtoto wake Ikram. 

"Nafasi ya Mama Ikram katika moyo wangu ni kubwa sana kwa sababu kipindi nilikuwa naanza sanaa alikuwa ananisapoti sana. Mama Ikram ni special," Alisema katika mahojiano.

Aliongeza kuwa mtoto ambaye alipata na Bi. Rukia ni ,"Mwanangu wa dhahabu."

Haya yanajiri siku chache tu baada yake kufunguka kuhusu tatizo hatari la moyo ambao huenda ukafanya asiweze kupata watoto wengine atimizapo umri wa miaka 30.

"Daktari aliniambia shida yangu huenda ikawa kubwa zaidi  baada ya kufikisha miaka 30. Alisema huenda ikanipelekea nisipate tena watoto nisipofanya matibabu," Alisema katika mahojiano na Wasafi Media.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 29 alifichua kuwa amekuwa akipambana na hali hiyo kwa kipindi kirefu.

Mbosso alieleza kuwa hali hiyo inayofanya mwili wake kutetemeka imesababishwa na  kuziba kwa mishipa yake.

"Nimeambiwa matatizo yangu yanatokana na mishipa yangu ya damu kuzibwa na mafuta. Hali hii haijanipata ukubwani, ni tangu nizaliwe," Mbosso alisema.

Mwanamuziki huyo alisema atasafiri kuenda kutibiwa baada ya kupanga mambo yake nyumbani kwani matibabu yatachukua muda mrefu.