"Ni sumu!" Babake Paula afunguka kuhusu uhusiano wake wa sasa na Kajala

Hakujakuwa na hali ya kuelewana kati ya P-Funk na Kajala.

Muhtasari

•P-Funk na Kajala walikuwa kwenye mahusiano takriban miongo miwili iliyopita na kubarikiwa na binti mmoja pamoja.

•P-Funk alidai kuwa Kajala amekuwa akipuuzilia ushauri  wake wote  hasa kuhusu malezi ya binti yao.

P-Funk Majani na Kajala Masanja
Image: HISANI

Mtayarishaji muziki P-Funk Majani amefichua kuwa uhusiano kati yake na mzazi mwenzake Kajala Masanja sio mzuri.

Wawili hao walikuwa kwenye mahusiano takriban miongo miwili iliyopita na kubarikiwa na binti mmoja pamoja, Paula Paul Kajala.

Akizungumza na waandishi wa habari Ijumaa, P-Funk alifichua kuwa kwa sasa hata hazungumzi na muigizaji huyo.

"Mama (Kajala) ni sumu. Lazima izingatiwe niko kwenye ndoa miaka nane na mtu ambaye nimekuwa naye miaka 12, kanizalia watoto watatu. Sasa kama mtu ako na drama unaepuka kidogo," P-f=Funk alisema.

Mtayarishaji huyo alifichua kuwa kwa muda mrefu hakujakuwa na hali ya kuelewana kati yake na Kajala.

Alidai kuwa mchumba huyo wa sasa wa Harmonize amekuwa akipuuzilia ushauri  wake hasa kuhusu malezi ya binti yao.

"Paula bado mdogo, ana nafasi ya kubadilisha tabia. Mama yake yule hapana. Kwa kweli sisi hatuongei. Sihitaji kuongea naye tena!," Alisema.

P-Funk hata hivyo alibainisha kuwa uhusiano kati yake na huyo wao mwenye umri wa miaka 20 ni mzuri. Alidokeza kuwa yeye na Paula hujuliana hali mara kwa mara na hata kukutana kwa wakati mwingine.

Mtayarishaji huyo alimtakia bintiye kila la kheri wakati akiadhimisha siku ya kuzaliwa mnamo Ijumaa (Julai 15).

Alipongeza maendeleo ya mwanamitindo huyo chipukizi na kumtaka afuate moyo wake katika shughuli zote za maisha.

"Nipo kwa ajili yake siku zote. Siku hizi tunaongea vizuri sana. Tunaenda vizuri na amekua. Ameanza kuwa mzima,"

Mnamo Ijumaa Paula alitimiza miaka 20. 

Ili kumsherehekea, Kajala aliweka bango kubwa barabarani lenye sura ya bintiye na ujumbe wa kheri za siku ya kuzaliwa.

"Kheri za siku ya kuzaliwa Paula. Mama anakupenda," Maandishi ya bango hilo yalisoma.

Huku akisherehekea jambo hilo Paula alikiri upendo wake mkubwa kwa mama yake na pia  baba yake.

"Asante kwa mama yangu na baba. Nawapenda. Angalieni jameni, mnaniona," Paula alisikika akisema katika kanda ya video aliyopakia Instagram. 

Kwa sasa mwanamitindo huyo ni mtoto wa kambo wa Harmonize ila kumekuwa na tetesi nyingi kuwa hakuna uhusiano mzuri kati yao.