(Video) "Oa mke ambaye unaweza mkumbatia wakati ana hasira," - Mchungaji Elizabeth Mokoro

mchungaji huyo alikuwa katika ibada ya kuhubiri ya mchana katika kanisa la SDA, Kisii.

Muhtasari

• Alisema mke anayepiga kelele akizunguka nyumba nzima anaweza kutulizwa tu kwa kumbato moja la nguvu, na kuwataka wanaume kuoana wanawake wanaweza kumbatia kwa nguvu.

Mhubiri mmoja wa dhehebu la SDA kwa mara nyingine tena katiba ibada moja ya kanisani ametoa ushauri kwa wanandoa kuhusu jinsi ambavyo wanafaa kuishi katika nyumba moja kwa amani isiyomithilika.

Katika video moja ambayo imesambazwa mitandaoni, mchungaji huyo kwa jina Elizabeth Mokoro anasema kwamba mwanaume unafaa kumuoa mwanamke amabye unamuelewa ndani nje haswa wakati wa hasira zake kwa sababu hilo litakusaidia kumthibiti vilivyo.

“Elewa nguvu ya kugusa ndio ukiwa na mke ambaye hawezi nyamaza na kufunga mdomo waakti wa hasira zake, anapiga kelele akielekea jikoni, akirudi kuelekea chumba cha kulala, anapakua chakula sebuleni bado akiendelea kunung’unika, mwanamke kama huyo unamngoja kwenye ukanda ambapo ni sehemu nyembamba na finyu, halafu unamkumbata kwa sana,” mchungaji Mokoro anaonekana akihubiri kwenye video moja iliyosambazwa mitandaoni.

Kulingana na mchungaji huyo, nguvu ya kushika na kugusa mtu kwa mahaba hapo ndio inakujia kwani baada ya kumshikilia kwa kumbato la nguvu mke wake mwenye kupiga kelele za hamaki huku na kule, atahisi upendo wako na hapo utamuona kanywea kweli kweli na kuwa laini kama ini lililopikwa.

“Mshikilie kwa nguvu kabisa, ndio maana nasema oa mtu ambaye unaweza ukashikilia. Ataanza kukuambia niachilie, usinishike halafu ukali wake utapoa kadri unavyoendelea kumshikilia kwa nguvu, halafu muangalie machoni moja kwa moja umuulize mbona anapiga kelele, utasikia kwa upole akikujibu tatizo ni lipi,” mchungaji huyo alielezea kwa ucheshi mkubwa.

Katika video nyingine, mchungaji huyo alionekana akishauri wanawake ambao wameoleka na watu ambao ni wadogo kuwaliko huku akiwataka kukimbia kutoka kwa hayo mahusiano kwa sababu ni kama kujidanganya tu. Kulingana na yeye, mwanaume siku zote sharti awe mkubwa kiumri kuliko mwanamke.