'Ninajisamehe kwa kutokuwa mkamilifu,' Jimal azungumza baada ya Amira kujibu ombi la msamaha

Jimal alialika drama nyingi kwenye ndoa yake baada ya kujitosa kwenye mahusiano na Amber Ray

Muhtasari

•Ujumbe wa Jimal  wa hivi punde umeonekana kuwa mwendelezo wa majuto yake kwa kuvunja ndoa yake.

•Amira alisema kwa sasa hawezi kuuelewa msamaha wa mumewe kwani ulifufua kumbukumbu ya siku mbaya za nyuma.

katika picha ya zamani
Jimal Rohosafi na Amira katika picha ya zamani
Image: HISANI

Ni wazi kuwa Mwenyekiti wa Muungano wa Wamiliki wa Matatu jijini Nairobi Jimal Rohosafi kwa sasa ni mtu mwenye majuto kufuatia makosa yake ya awali.

Mwaka jana, Jimal alialika drama nyingi kwenye ndoa yake na kuzungumziwa sana mitandaoni baada ya kujitosa kwenye mahusiano ya kimapenzi na mwanasoshalaiti Amber Ray, hatua ambayo sasa anakiri kujutia.

Wikendi mfanyibiashara huyo alichukua hatua ya kuomba msamaha kwa mkewe kufuatia masaibu aliyomsababishia.

"Wengi wenu, kama si wote mnajua kilichotokea kati yangu na mke wangu na jinsi tulivyojulikana; Kwa kusema kidogo, Ilikuwa chafu! ilikuwa ya fujo! ilikuwa mbaya kabisa! Niliweza kuonekana kutosumbuliwa lakini sikuwa na la kufanya, nilijua ni makosa, nilijua unaumia lakini sikuweza kujikusanya! Amira ninafanya hivi kwa sababu kukukosea  heshima pia kulikuwa kukubwa. Naomba radhi kwa kutoheshimu, kwa aibu yote, kwa maudhi yote, kwa maumivu yote, 💔Samahani kwa nyakati zote ambazo sijawa mwanaume niliyeahidi kuwa," Jimal alimuambia mkewe kupitia Instagram.

Mfanyibiashara huyo alikiri kuwa alikosa kutimiza  wajibu wake wa kumlinda mkewe kama alivyohitajika kufanya.

Pia alikiri kwamba hajakuwa sawa tangu alipokosana na mke huyo wake na mama ya watoto wake. Alidokeza kuwa yupo tayari kupiga hatua zozote ili kufufua ndoa yao iliyokufa miezi kadhaa iliyopita.

"Tafadhali nisamehe. Mimi na wewe tumetoka mbali na kukupitishia kwa yote hayo hakukuwa kuzuri. Tafadhali nisamehe Amira," Aliandika.

Takriban siku mbili baadae Amira hatimaye alijibu ombi hilo la msamaha  huku akiweka wazi kuwa haitakuwa jambo rahisi kusahau maumivu ambayo baba huyo wa watoto wake alimsababishia.

Amira alisema kwa sasa hawezi kuuelewa msamaha wa mumewe kwani ulifufua kumbukumbu ya siku mbaya za nyuma.

"Ombi hilo la msamaha limenirudisha katika sehemu moja ya giza ambayo nimewahi kuwa katika maisha yangu kwa sababu nimetafakari juu ya mengi yaliyotokea hadharani na nyuma ya milango iliyofungwa na imezua hisia nyingi,"

"Vidonda vingine haviponi, lazima ujifunze jinsi ya kuishi navyo," Aliandika Amira.

Mwanzoni Jimal alisalia kimya baada ya jibu hilo la mkewe lakini sasa ameonekana kuvunja ukimya na kukiri kuwa si mtu kamilifu.

"Ninajisamehe kwa kutokuwa mkamilifu," Jimal ameandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Ujumbe huo wake wa hivi punde umeonekana kuwa mwendelezo wa majuto yake kwa kuvunja ndoa yake.

Ndoa ya Jimal ilivunjia miezi kadhaa iliyopita baada yake kumchagua Amber Ray dhidi ya mama huyo wa watoto wake.