"Siko soko!" Carol Muthoni athibitisha mahusiano mapya baada ya kutengana na Mulamwah

Muthoni amedokeza kuwa tayari amesonga mbele kutoka kwa mahusiano yake na Mulamwah.

Muhtasari

•Muthoni amedokeza kuwa sasa yupo katika mahusiano mengine baada ya kutengana na mchekeshaji huyo.

•Mapema mwezi huu,  muigizaji huyo kwa mara ya kwanza alimtambulisha jamaa anayeaminika kuwa mpenzi wake mpya.

Carrol Sonnie katika studio za Radio Jambo
Carrol Sonnie katika studio za Radio Jambo
Image: RADIO JAMBO

Muigizaji Carol Muthoni ameendelea kuonyesha ishara zaidi kwamba tayari amesonga mbele kutoka kwa mahusiano yake wa awali na Mulamwah.

Muthoni amedokeza kuwa sasa yupo katika mahusiano mengine baada ya kutengana na mchekeshaji huyo.

Katika kipindi cha Maswali na Majibu kwenye Instagram, shabiki mmoja alimuuliza kwa nini amekataa kuchumbiana naye.

"Mbona hunitaki?" Shabiki aliuliza.

Bila kusita Muthoni alijibu , "Juu siko soko."

Kwa lugha ya mtaani nchini Kenya "kuwa soko" ina maana kwamba mtu hayupo katika mahusiano na yupo huru kuchumbiwa.

Kinyume chake, "siko soko" ina maana kuna uwezekano mkubwa kuwa tayari mtu yupo katika mahusiano au ndoa.

Mwishoni mwa mwaka jana Muthoni na Mulamwah walitangaza kutengana kwao, miezi mitatu tu baada ya binti yao kuzaliwa.

Akithibitisha kutengana kwao, Muthoni alifichua kuwa walikubali kwenda njia tofauti kwa sababu zao za kibinafsi.

"Hii ni kuweka wazi kuwa mimi na Mulamwah hatuko pamoja tena. Sote tumekubaliana na tumeamua kuachana kwa sababu tunazozijua sisi. Asante sana kwa upendo na usaidizi ambao mliotupa katika kipindi cha miaka hiyo 4 ambacho kimepita, mimi binafsi siichukulii kawaida. Kwa Mulamwah, asante sana kwa kuniruhusu kuwa sehemu ya maisha yako miaka hiyo. Nashukuru sana na nitahifadhi kumbukumbu milele. Katika hatua yako inayofuata maishani, sikutakii chochote kingine ila bora zaidi. Endelea kushinda na Mungu akubariki katika kila hatua ya maisha yako," Muthoni alitangaza kupitia Instagram.

Baadae uhusiano kati ya wasanii hao wawili ulizidi kudhoofika huku wakinyoosheana vidole kuhusu kuvunjika kwa mahusiano yao.

Takriban miezi miwili iliyopita wazazi wenza hao walidhaniwa kurudiana baada ya kupakia video na picha wakiwa pamoja. Hata hivyo baadae walikana madai ya kurudiana.

Katika siku za hivi majuzi Muthoni amekuwa akidokeza mahusiano mapya ingawa bado hajamfichua mpenzi wake mpya.

Mapema mwezi huu,  muigizaji huyo kwa mara ya kwanza alitambulisha jamaa anayeaminika kuwa mpenzi wake mpya.

Muthoni alipakia video iliyoonyesha akipapasa mkono wa mwanaume aliyefichwa sura ambaye alikuwa akiendesha gari.

Siku chache baadae mpenzi huyo wa zamani wa Mulamwah alipakia video zingine zilizoonyesha akijivinjari hotelini pamoja na mwanaume huyo.

"Wacha leo nimspoil na pesa yake." Aliandika chini ya video moja.

Kufikia sasa hatujaweza kumtambua mpenzi mpya wa muigizaji huyo kwa bado hajaifichua sura yake kamili.