"Niko hapa kwa sababu nataka kuwa!" Zari Hassan atetea mahusiano yake na kijana mdogo

Zari aliwataka watu kusita kuhoji kuhusu kazi na uwezo wa kifedha wa mpenziwe.

Muhtasari

•Mama huyo wa watoto watano alitangaza wazi kuwa maisha yake hayafungwi na sheria zilizowekwa na jamii.

•Zari aliwataka watu kusita kuhoji kuhusu kazi na uwezo wa kifedha wa mpenziwe.

Image: INSTAGRAM// ZARI HASSAN

Mwanasoshalaiti maarufu Zari Hassan hatimaye amevunja kimya chake na kuwajibu watu ambao wamekuwa wakimkosoa kwa kuchumbiana na mwanaume mwenye umri mdogo kuliko yeye.

Akizungumza kwenye video ambayo alipakia, Zari ambaye alionekana kughadhabishwa sana alisema yuko na haki kamili ya kumchagua yule ambaye angependa kuchumbiana naye.

Mama huyo wa watoto watano alitangaza wazi kuwa maisha yake hayafungwi na sheria zilizowekwa na jamii.

"Ukiniambia nichumbie nani na nisichumbie nani, nawajua wa aina hizo. Lakini hapa ndipo ninapoamua kubaki. Ni nini kinachokufanya ufikiri kwamba watu wengine hawana hadhi?,"  Zari alisema.

Mpenzi huyo wa zamani wa Diamond Platnumz aliwataka watu kusita kuhoji kuhusu kazi na uwezo wa kifedha wa mpenziwe.

Alibainisha kwamba uamuzi wa nani wa kuchumbiana uko kwake na sio kwa wale ambao wanakosoa hatua zake.

"Niko hapa kwa sababu nataka kuwa hapa, sio kwa sababu mnataka kunichagulia mahali pa kuwa," Alisema.

Zari amekuwa akikejeliwa na kukosolewa sana baada ya kufichua mpenzi wake wa sasa takriban mwezi mmoja uliopita.

Alionekana na mpenzi huyo wake kwa mara ya kwanza katika ziara ya kikazi nchini Kenya na Tanzania.

Akiwahutubia waandishi wa habari baada ya kutua Tanzania, Zari alimtambulisha mwanaume huyo, sio tu kama mpenzi wake, bali pia kama mume wake.

“Huyu ni mume wangu, ni mume wangu, kesi kwisha!” Zari alisema

Mzaliwa huyo wa Uganda hata hivyo alikataa kufichua jina la mpenzi  wake wakati alipoombwa kufanya vile.

Wiki mbili zilizopita Zari alizamia kwenye Instagram kueleza jinsi anavyommiss mpenzi wake baada ya kuwa mbali naye kwa muda.

Kwenye Instastori zake alipakia picha ya jamaa huyo ambaye ni machache tu yanayojulikana kumhusu na kudokeza jinsi anavyotamani angekuwa karibu.

"Miss you!" Zari aliandika

Isitoshe, mfanyibiashara huyo kutoka Uganda alifuatisha ujumbe wake na emoji inayoashiria mtu mpweke.