Pritty Vishy amshauri Stivo Simple Boy baada ya kuvisha mpenziwe pete ya uchumba

Vishy alimsihi Stivo kuendeleza urafiki naye licha ya kuwa walitengana miezi kadhaa iliyopita.

Muhtasari

•Pritty Vishy alikosoa jinsi aliyekuwa mpenziwe Stivo  Simple Boy alivyoomba ndoa kwa anayedaiwa kuwa mpenzi wake.

•Pia alimsihi kuendeleza uhusiano mzuri wa kirafiki naye licha ya kuwa walitengana miezi kadhaa iliyopita.

Stivo Simple Boy na aliyekuwa mpenzi wake Pritty Vishy
Stivo Simple Boy na aliyekuwa mpenzi wake Pritty Vishy
Image: SCREENGRAB// MUNGAI EVE

Wikendi, msanii tajika kutoka Kibra Stivo Simple Boy anadaiwa kumvisha pete ya uchumba  mpenzi wake mpya.

Video iliyosambazwa  kwenye mitandao ya kijamiiJumatatu  ilimuonyesha rapa huyo akimuomba ndoa kipusa anayedaiwa kuwa mpenzi wake, Jenny Wangui.

Mwanadada huyo alikubali ombi la Stivo na marafiki wachache waliokuwa pale wakaonekana wakishangilia hatua hiyo.

Kuvishana pete ya uchumba kwa Stivo kulialika hisia mseto kutoka kwa wanamitandao huku baadhi yao wakimpongeza, wengine wakimkosoa na wengine hata wakiibua madai kuwa ni kiki tu.

Aliyekuwa mpenzi wake, Pritty Vishy ni miongoni mwa waliompongeza kwa hatua kubwa ambayo alipiga.

"Kusema kweli nina furaha kwa ajili yao. Mimi nina furaha sana kwa ajili yake (Stivo) kwa sababu ata nilimove on. Kila mtu amemove on," Vishy alisema katika mahojiano na Eve Mungai.

Mrembo huyo mwenye umri wa miaka 20 hata hivyo alikosoa jinsi Stivo alivyoomba ndoa kwa anayedaiwa kuwa mpenzi wake.

Alisema kuwa hatua hiyo ya kuvishana pete ya uchumba haikupangwa vizuri na haikuendelezwa kwa njia mwafaka.

"Hiyo proposal haikupangwa. Utatangaza aje ati unaenda kupropose? Si proposal huwa surprise?! Kitu cha pili, itakuwaje kundi la wanaume iko hapo na ya wanawake hapo alafu kijana (Stivo) anaongelesha, kidogo kidogo msichana anagongwa kwa bega kidogo anaombwa ndoa. Hata hivyo mimi sina shida, nina furaha kwa ajili yao," Alisema.

Vishy alimshauri mpenzi huyo wake wa zamani kuwa makini kuhusu masuala ya mahusiano na ndoa.

Pia alimsihi kuendeleza uhusiano mzuri wa kirafiki naye licha ya kuwa walitengana miezi kadhaa iliyopita.

"Ningependa awe rafiki yangu. Juu tuliachana haimaanishi tunafaa kuwa maadui. Huwezi kujua huko mbele tutasaidiana vipi. Ningependa awe rafiki yangu na apate mtu bora zaidi," Alisema.

Pia alimshauri Stivo kumdekeza mchumba huyo wake wa sasa na kumuonyesha mapenzi jinsi ambavyo wanadada hupenda.

Aidha alimuomba mchumba wa Stivo kumfundisha  mahaba na kumuelekeza kuhusu jinsi ambavyo angependa kutunzwa.

"Siwezi penda kukosa harusi yake (Stivo). Ningependa kumuona mwanamke akisema ndio na yeye pia akisema ndio na wakikumbatiana. Nina furaha sana, mimi ningependa kuhudhuria," Alisema Vishy.

Vishy pia alisisitiza kuwa yupo kwenye mahusiano ya kweli na mwanamuziki Madini Classic, japo wengi wamekuwa wakiyatilia shaka.