Choo kimoja cha umma jijini Nairobi kinapiga muziki kuwaburudisha wateja wanapojisaidia

Mhudumu wa choo alisema waliamua kuweka huduma hiyo kama njia moja ya kutoa msongo wa mawazo kwa wateja

Muhtasari

• "Hii ni tafrija tunayowapa wateja wetu... na tumekuwa tukicheza muziki kwenye choo chetu kwa muda sasa..." mhudumu wa wateja alisema

Choo cha umma katikati mwa jiji kuu la Nairobi
Choo cha umma katikati mwa jiji kuu la Nairobi
Image: The Star//Maktaba

Baadhi ya wahudumu wa vyoo vya umma jijini Nairobi wameamua kuimarisha huduma kwa wateja wao kwa kuwawekea miziki katika vituo vyao vya huduma za kujisaidia.

 

Kulingana na taarifa zilizochapishwa kwenye wavuti wa kituo kimoja cha habari humu nchini, Kati ya vyoo 18 vya umma jijini Nairobi kuna choo kimoja maalumu, kilicho kando ya barabara ya Tom Mboya, ambacho kimekuwa kikiwatumbuiza wageni wake kwa muziki wakuwabamba wateja huku wakiendelea na shughuli hiyo muhimi ya kibaolojia.

 

Wakati vipaza sauti vikiwa vimewekwa pasiko onekana, Mhudumu huonekana ameketi kwenye kona, akicheza nafasi ya 'DJ' kwa kuchanganya aina tofauti za muziki kulingana na wakati wa siku, hisia na bila shaka orodha zao zimekuwa zikiwabamba vilivyo wateja wao, kulingana na ripoti walizopata kutoka kwa baadhi waliojaribu kuuliza miziki hiyo imeimbwa na nani baada ya kumaliza shughuli ya kujisaidia.

 

"Hii ni tafrija tunayowapa wateja wetu... na tumekuwa tukicheza muziki kwenye choo chetu kwa muda sasa..." mhudumu wa wateja alinukiliwa akijibu kwenye Mahojiano na chombo kimoja cha habari aliyetaka kujua ni kwa nini huduma hiyo imejumuishwa katika sehemu hizo.

 

“Watu wanapenda muziki, na tunaamini kucheza aina tofauti za muziki kunaweza kusaidia kutoa msongo wa mawazo,” aliongeza mhudumu huyo, kulingana na nukuu katika wavuti huo.

 

Alipoulizwa kama wanacheza muziki kila wakati, Njeri anasema: "Hapana, si kila wakati. zaidi nyakati za jioni, siku za wiki hasa, tunapokuwa na wateja wengi."

 

Kulingana na taarifa hiyo, hadi wateja wa vyoo hivyo walifikiwa ili  kutoa wazo lao kuhusu huduma hiyo na mmoja aliyezungumza alisema kuwa muziki huo ni nyongeza nzuri kwani unaifanya sehemu hiyo kuwa na uchangamfu kidogo.

Kwa upande wake, Njeri anabainisha kuwa pengine ni kituo chao pekee kinachocheza muziki, kuwaburudisha wateja, kuwarejesha hisia zao wanapoendelea na biashara zao kwenye sehemu hiyo waliopo.

Maeneo mengi humu nchini, vyoo vya kulipa ambavyo aghalabu hupatikana maneneo ya miji na masokoni hulipisha gharama ya shilingi 10 tu pesa za benki kuu ya Kenya, na moja kati ya biashara inayong’ang’aniwa sana katika usimamizi haswa jijini Nairobi ambapo miaka michache nyuma paliibuka makundi hasimu waliokuwa wakipigania usimamizi wa vyoo vilivyopo katika eneo moja jijini. Hii ni kutokana na hela nzuri zinazokusanywa kila siku kutoka biashara hiyo kwani mtu huwezi kupigania kitu usichoona faida yake.