Bango la Kajala na Harmonize latundikwa katika kilele cha Mlima Kilimanjaro

Kajala alishindwa kuzuilia hisia baada ya bango lake na Harmonize kufungwa katika kilele cha mlima mrefu zaidi Afrika.

Muhtasari

•Bango hilo lilifungwa kwenye ishara  ya mwelekeo katika Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro iliyo kileleni cha mlima huo.

•Picha iliyo kwenye bango hilo ilipigwa wakati Harmonize alipomvisha muigizaji huyo pete ya uchumba.

mnamo siku ya kuvisha pete ya uchumba
Harmonize na Kajala mnamo siku ya kuvisha pete ya uchumba
Image: INSTAGRAM// KAJALA MASANJA

Bango la wachumba Harmonize na Kajala Masanja limetundikwa katika kilele cha Mlima mrefu zaidi barani Afrika.

Alhamisi, Kajala alipakia picha zilizoonyesha wakwea milima wawili wakisimama kando ya bango lenye sura yake na mpenziwe katika kilele cha Mlima Kilimanjaro.

"Harmonize na Kajala Hongera!" Bango hilo lilisoma.

Bango hilo lilifungwa kwenye ishara  ya mwelekeo katika Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro iliyo kileleni cha mlima huo.

"Love❤❤" Kajala alisherehekea chini ya picha moja.

Picha iliyo kwenye bango hilo ilipigwa wakati Harmonize alipomvisha muigizaji huyo pete ya uchumba.

Image: INSTAGRAM// KAJALA MASANJA

Mwishoni mwa mwezi Juni, Kajala alikubali ombi la ndoa la staa huyo wa Bongo na kuvishwa pete ya uchumba. 

Haya yalijiri takriban mwezi mmoja tu baada yao kurudiana baada ya kutokuwa na uhusiano mzuri kwa mwaka mmoja.

Akitoa hotuba yake baada ombi lake la ndoa kukubalika, Harmonize  alisimulia jinsi mama huyo wa binti mmoja alivyomkaribisha kwake wakati alipokuwa akipitia kipindi kigumu sana cha maisha yake.

"Umekuwepo kwa ajili yangu katika mambo mengi ambayo siwezi kueleza hivi sasa. Ni siri kati yangu na wewe na hata mara zingine umeniambia nisiseme hadharani. Kuna wakati nilikuwa napatia wakati mgumu hata ukanichukua, nikaishi nyumbani kwako na ni hivi majuzi. Sikuwa na nyumba au hata pa kulala... na hiyo imekuwa siri kati yangu na wewe na umeificha, hujai kuzungumzia mtu yeyote," Alisema.

Katika kipindi cha miezi miwili ambacho kimepita wachumba hao wameonekana kufurahia maisha pamoja huku Harmonize hata akiahidi kumuoa muigizaji huyo.

Wakati akimsherehekea mnamo siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwake, Harmonize aliahidi kumuoa mchumba huyo wake hivi karibuni na hata kuapa kutochepuka hata kidogo.

“Kheri njema ya siku yako ya kuzaliwa mpenzi wa maisha yangu MISS BANTU. Kukuoa ni ndoto na nashukuru Mungu tunakaribia hapo. Kukufanya meneja wa kazi zangu za kimuziki inaonesha kiasi gani nakuamini na kiasi gani wewe ni wa muhimu katika maisha yangu. Najua wengi wanakubeza, wengi hawaamini kwamba unaweza simama imara. Katika kazi hii yenye ugumu wake, ndio wewe unaweza,” Harmonize aliandika kwenye Instagram

Wasanii hao wa Bongo walikuwa wametengana Aprili mwaka jana huku uvumi mwingi kuhusu sababu ya kutengana ukienea. Walikuwa wamechumbiana kwa kipindi cha miezi michache tu kabla ya kutengana.