Mkewe Weasel azungumzia madai madai ya kupigwa na mumewe

Kaka huyo wa Chameleone anadaiwa kumpa mkewe kichapo cha mbwa na kumharibu uso.

Muhtasari

•Mwanasoshalaiti Sandra Teta amejitokeza kupuuzilia mbali madai ya kudhulumiwa kimwili na mumewe.

•Weasel amethibitisha kuwa mkewe anaendelea kupokea matibabu nyumbani na ameanza kupata afueni.

Bi Teta Sandta na mumewe Weasel Manizo
Image: HISANI

Mke wa mwimbaji wa Uganda Weasel Manizo hatimaye amejitokeza kupuuzilia mbali madai ya kudhulumiwa kimwili na mumewe.

Siku ya Alhamisi, picha zilizomuonyesha Miss Sandra Teta akiwa amevimba usoni zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii na ikadaiwakuwa sura yake ilikuwa imeharibiwa kutokana na kichapo kikubwa alichopokea kutoka kwa mumewe Weasel.

Ripoti kutoka Uganda zilisema kuwa mwanamitindo huyo kutoka Rwanda alikuwa akiuguza majeraha nyumbani baada ya Weasel kumshambulia huku Waganda wakizamia mitandaoni kukashifu kitendo hicho.

"Mwimbaji Weasel anaripotiwa kumpiga mpenzi wake Sandra Teta. Kwa sasa anauguza majeraha," Ripoti ya kituo kimoja cha habari nchini Uganda ilisoma.

Bi Teta hata hivyo amekana madai ya kupigwa na kaka huyo wa Chameleone na badala yake kueleza kuwa uso wake uliharibiwa baada ya kushambuliwa na wezi.

Alisema anaendelea  kupokea matibabu nyumbani baada ya kuvamiwa na wezi walioiba simu yake, mkoba na shilingi milioni 1.3 za Uganda ambazo alikuwa amebeba Ijumaa usiku.

"Kwa kurejelea picha zilizosambaa kwenye Vyombo vya Habari, nikiwa njiani kutoka kazini Ijumaa usiku, nilivamiwa na majambazi wasiojulikana ambao walikimbia na simu yangu, mkoba na Ush1.3M. Kwa muda wa wiki moja iliyopita nimekuwa kwenye matibabu na ninaendelea kupata nafuu," Teta alisema kupitia Instagram.

Msanii Weasel pia amethibitisha kuwa mkewe anaendelea kupokea matibabu nyumbani na tayari ameanza kupata afueni.

Baadhi ya wanamitandao hata hivyo wameendelea kutilia shaka jambo hilo huku wakisisitiza kuwa mwimbaji huyo alimpiga mkewe.

Weasel na kipusa huyo kutoka Rwanda walianza kuchumbiana mwaka wa 2018 na wamepanga kufunga pingu za maisha baadae mwaka huu.

Wawili hao tayari wamebarikiwa na watoto wawili pamoja.