Hivi karibuni! Jux afunguka kuhusu mipango yake ya ndoa

"Ndoa ni kitu kizuri. Nitafunga ndoa hivi karibuni. Mtajua ikifika," Jux alisema.

Muhtasari

•Jux ameweka wazi kuwa anaithamini sana ndoa na kubainisha kuwa anakusudia kupiga hatua hiyo.

•Mapema mwaka huu, Jux alidaiwa kuwa kwenye mahusiano na kipusa wa Rwanda aliyetambulishwa kama Karen.

Huddah Monroe na Juma Jux
Huddah Monroe na Juma Jux
Image: INSTAGRAM// JUMA JUX

Staa wa Bongo R&B Juma Jux amedokeza kuwa anapanga kufunga ndoa na mpenzi wake hivi karibuni.

Jux ameweka wazi kuwa anaithamini sana ndoa na kubainisha kuwa anakusudia kupiga hatua hiyo.

"Ndoa ni kitu kizuri. Nitafunga ndoa hivi karibuni. Mtajua ikifika," Jux alisema katika mahojiano na waandishi wa habari.

Mpenzi huyo wa zamani wa Vanessa Mdee hata hivyo hakumfichua mchumba wake ambaye anakusudia kuoa.

"Tutafika muda mtamjua," Alisema.

Mwimbaji huyo mwenye kipaji cha kuheshimika kweli amekuwa msiri sana kuhusu mahusiano yake ya sasa.

Mapema mwaka huu, Jux alidaiwa kuwa kwenye mahusiano na kipusa kutoka Rwanda aliyetambulishwa kama Karen.

Karen aliripotiwa kuwa mpenzi wa mwanamuziki huyo baada ya kuoneka akiendesha Benz yake  na hata kutembea kwake usiku.

Malkia huyo hata hivyo alidaiwa kumtema Jux kufuatia uhusiano wake wa kutiliwa shaka na mwasoshalaiti wa Kenya Huddah Monroe.

Katika kipindi cha takriban miezi miwili ambacho kimepita kumekuwa na tetesi nyingi kuwa Jux anachumbiana na Huddah. 

Madai kuwa wawili hao wanachumbiana yalivuma zaidi baada ya kuonekana wakibusu hadharani mara kwa mara.

Hata hivyo wasanii hao tayari wamejitokeza kueleza kuwa uhusiano wao ni wa kirafiki ila sio wa kimapenzi.

"Mimi nipo kwenye mahusiano na najua Huddah yuko kwenye uhusiano wa kimapenzi. Kwahiyo swala la sisi wawili kuwa wapenzi halijitokezi. Lakini nitalijibu swali hili siku nyingine. Lolote linaweza kutokea." Jux alisema katika mahusiano ya hapo awali.

Jux aliwahi kuwa kwenye mahusiano marefu na mke wa sasa wa muigizaji Rotimi kutoka Marekani, Vanessa Mdee.

Jux alichumbiana na Vanessa kwa takriban miaka sita ila mahusiano yao yakagonga mwamba mwaka wa 2019. Miezi kadhaa baadae Vanessa alijitosa kwenye mahusiano na Rotimi kutoka  ambaye tayari wana mtoto mmoja pamoja.