(+Video) Magoha amlikwa kwa kumfokea jamaa "Wewe unanuka chang'aa enda mbali na mimi!"

Waziri Magoha alikuwa akishiriki upanzi wa micje katika shule moja

Muhtasari

• Waziri Magoha kwa mara nyingine tena amejipata katika vita vya maneno na wanamitandao kwa kumfokea jamaa kwamba ananuka pombe.

• Juzi alizua gumzo baada ya kumuuliza mwanahabari wa Kiislamu kama yeye ni mshirika wa Al Shabaab.

Waziri wa elimu profesa George Magoha kwa mara nyingine tena amejipata katika vita vya maneno na watumizi wa mitandaoni baada ya kuonekana akimdunisha jamaa mmoja aliyekuwa anamsaidia kushika jembe ili apate nafasi ya kunyunyizia miti wakati wa hafla ya upanzi wa miti katika shule moja.

Katika video ambayo ilisambazwa na kuzua gumzo pevu kwenye mtandao wa Twitter, Magoha anaonekana akishirikiana na wanafunzi katika shughuli hiyo ya upanzi wa miti huku machifu na umati wa watu wanaodhaniwa kuwa wazazi ukiwa umemzingira kushuhudia tukio hilo lenye kuleta tija kwa jamii.

Jamaa huyo alipomsogelea karibu Waziri Magoha, Waziri huyo ambaye kutabasamu kwake ni nadra kama kumpata mwanasiasa aliye muaminifu ashakum si matusi anaonekana akimfokea kwa ukali huku akisema kwamba ananuka kileo aina ya chang’aa na kumuonya vikali asimkaribie.

“Wewe, unanukaa changaa, Kwenda mbali kabisa na mimi. Sichezi na wewe,” Magoha anamfokea huku akichukua kibuyu chenye maji na kuendelea kunyunyizia miche hiyo iliyopandwa.

Video hiyo ilizua maoni kinzani miongoni mwa Wakenya kwenye mtandao wa Twitter huku wengine wakishangaa jinsi anavyowafanya watu wanaofanya kazi chini ya wizara yake, haswa mbali ya kamera.

Wengine walichukua nafasi hiyo kutolea ushuhuda jinsi ambavyo waliwahi kumuona akiwafanyia watu katika baadhi ya hafla alizohudhuria.

“Nilihudhuria hafla ya kuapishwa kwa wajumbe wa bodi ya moja ya vyuo vikuu vya ndani na alimdhalilisha mmoja wa maprofesa kutokana na uvaaji wake. Magoha alimuuliza msomi huyo kuwa yeye ni nani na kama kweli alikuwa profesa, ilhali hakuweza kuvaa vizuri,” mmoja kwa jina Simon Peter Murimi aliandika kwenye video hiyo ya Twitter.

Wengine walimtetea Waziri Magoha na kusema kwamba watu wengi hawapendi kukaribiana na walevi wanaonuka vileo vya aina hiyo, hata ndani ya magari ya usafiri wa umma huwa wanafokewa na kuchukiwa na hakuna kikubwa kinachotendeka lakini kwa sabaabu ni wazxiri Magoha sasa watu wanawakisha ndimi za moto kutema cheche dhidi yake.

Hii si mara ya kwanza Waziri huyo amejipata kuwa gumzo kwenye mitandao kwani wiki jana alionekana tena kwenye video nyingine akimdadisi mwanahabari wa dini ya Kiislam huku akisaili kama kweli yeye ni mwanahabari ama ni mjumbe wa kundi lenye itikadi kali la Al Shabaab. Hili lilipokelewa na Wakenya wengi kwa mshtuko mkubwa kutoka kwa msomi huyo wa masuala ya udaktari na baada ya shinikizo kumkaba koo, ilibidi amesalimu amri na kuomba radhi kwa matamshi yake.