Nyahururu: Familia yabaki hoi mwili wa mpendwa wao kutoweka mochari, wapewa maiti nyingine

Familia hiyo ilisema ilipewa mwili mwingine ambao haukuwa wa mpendwa wao ambao ulikosekana.

Muhtasari

• Familia ilikataa mwili huo mbadala na kupiga ripoti katika kituo cha polisi huku mipango ya mazishi ikisitishwa.

Mwili wa marehemu ukisubiria kuzikwa
Mwili wa marehemu ukisubiria kuzikwa
Image: The Star// Jeneza

Familia moja katika kaunti ya Nyandarua imebaki katika hali ya sintofahamu baada ya mwili wa mpendwa wao kupotea kwa njia tatanishi kutoka makafani ya hospitali ya rufaa ya Nyahururu.

Kulingana na taarifa zilizochapishwa kwenye jarida moja la mitandaoni la humu nchini, familia ya mzee Raphael Ndung’u Ndisanjo mwenye umri wa miaka 72 ilifika katika mochwari ya hospitali hiyo walikokuwa wameuifadhi mwili wake lakini wakashangaa kupewa mwili tofauti na wa mpendwa wao. Walipojaribu kujua sababu za kupewa mwili tofauti na ule wa Ndisanjo, waliambiwa kwamba haukuweza kupatikana.

“Mwili uliowasilishwa kwetu na mhudumu wa chumba cha maiti haukuwa wa mpendwa wetu,” mjane wa marehemu alinukuliwa akilalama.

Kufuatia mkanganyiko huo, familia hiyo ilipiga ripoti katika kituo cha polisi ili utata huo upate kuzamiwa zaidi ya ukweli kuhusu kutoweka kwa mwili wa mzee Ndisanjo kupatikana.

Ndugu, jamaa na marafiki wa mzee waliojumuika kutoka janibu mbalimbali nchini walibaki katika hali ya mshangao huku kamati ya msiba huo ikilazimika kuahirisha mipango ya mazishi hadi pale mwili wa marehemu utakapopatikana.

Visa vya miili kupotea katika makafani na wengine kukabidhiwa miili ya watu ambao si jamaa wao vimekuwa vikiripotiwa sana nchini Kenya huku wengine wakilazimika kufukua miili ambayo walikuwa wameizika tayari na baadae kuambiwa kwamba marehemu waliyezika si jamaa wao kama walivyodhani.

Wiki jana familia moja katika kaunti ya Kakamega ilijipata katika mkwamo wa kifedha baada ya kusemekana kuzika mwili wa mtu waliyedhani ni mpedwa wao na siku mbili baada ya kuzika watu walijitoma kwao wakidai mwili huo ufukuliwe na kwamba ni wa mpendwa wao.

Familia hiyo ya Emmanuel Shamwata ilibaki ikilia kwa kusema kwamba walikuwa wametumia gharama kubwa zaidi ya laki 5 kwa mazishi ya Shamwata kwani alikuwa ni mchungaji wa kanisa zaidi ya 23.