Diamond Platnumz kutumbuiza mkutano wa kisiasa wa Raila Kasarani

Muhtasari

• Wanamuziki wengine wanaosemekana kutarajiwa kutumbuiza ni pamoja na msanii mkongwe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mbilia Bel

Msanii Diamond Platnumz ametajwa kuwa mmoja wa watumbuizaji katika hafla ya Azimio Kasarani
Msanii Diamond Platnumz ametajwa kuwa mmoja wa watumbuizaji katika hafla ya Azimio Kasarani
Image: Instagram//DiamondPlatnumz

Jumatano wiki hii, msanii namba moja wa muda wote Afrika Mashariki, Diamond Platnumz alitangaza ratiba yake na kusema kwamba Jumamosi hii angetumbuiza nchini Kenya kabla ya kujiandaa kweney matamasha mengine makubwa mwishoni mwa mwezi nchini Canada.

Sasa vyanzo vya habari na udaku karibu na msanii huyo vinadai kwamba huenda atakuwa mmoja wa watumbuizaji waalikwa katika hafla ya mkutano wa kisiasa wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya ambayo inaandaliwa katika uwanja wa Kasarani, sambamba na ile ya muungano pinzani wa Kenya Kwanza itakayofanyika Nyayo.

Jana Diamond Alipakia video kwenye kurasa zake akiwa na watoto wake na Zari nchini   Afrika Kusini ambapo alisema ilikuwa siku ya kuzaliwa ya mwanawe hii leo na mwanawe huyo alisikika kwenye video hiyo akimtaka baba mtu kumnunulia zawadi kochokocho kama vile simu ghali ya IPhone miongoni mwa zawadi nyingine.

Taarifa zinaeleza kuwa Diamond atakuwa nchini kwa ajili ya mkutano huo na kisha kurejea Afrika Kusini kwa ajili ya tafrija ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya mwanawe hiyo baadaye usiku wa leo.

Diamond alitumbuiza Nairobi mara ya mwisho mnamo Desemba 2018 wakati wa tamasha la Wasafi Festival kuadhimisha sherehe za Mwaka Mpya.

Mikutano ya kisiasa nchini Kenya inafikia kikomo hii leo kulingana na agizo la katiba linalotaka kampeni kukamilika angalau siku mbili kabla ya kuandaliwa kwa uchaguzi mkuu.

Uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika Agosti 9 ambayo ni siku mbili kutoka sasa na kinyang’anyiro hicho kimetajwa kuwa chenye ushindani kali kuwahi kutokea nchini tangu uhuru, wagombea wakuu wa urais Kinara wa Azimio la Umoja ambaye ni mwanasiasa wa muda mrefu Raila Odinga akijaribu karata kwa mara ya tano huku mpinzani wake mkubwa akiwa ni naibu wa sasa anayepeperusha bendera ya mrengo wa Kenya Kwanza, William Ruto.

Katika hafla ya Raila, wanamuziki wengine wanaosemekana kutarajiwa kutumbuiza ni pamoja na msanii mkongwe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mbilia Bel miongoni mwa wasanii tumbi nzima wa humu nchini.