Mke Ataka Talaka, Amtuhumu Mumewe Kujificha Chooni Wezi Walipovamia Nyumba Yao

Mwanamke huyo aliiambia mahakama kwamba hawezi endelea kuishi na mwanaume mwoga asiyeilinda familia yake dhidi ya hatari.

Muhtasari

• “Ni kweli nilijificha chooni wakati majambazi waliokuwa na silaha walipovamia nyumba yetu." mumewe alikiri.

Mwanamke anayetaka talaka
Mwanamke anayetaka talaka
Image: The star

Unaambiwa ukistaajabu ya Musa basi itakuwa bado hujayaona ya firauni!

Nchini Nigeria kuna taarifa imechapishwa na vyanzo vya habari ikisema kwamba mwanamke mmoja alielekea mahakamani akitaka mumewe kumpa talaka kwa kile alisema kwamba mumewe ni mtu mwoga.

Mwanamke huyo kwa jina Asiata Oladejo katika hati za mahakamani alisema kwamba hawezi kuendelea kuishi na mwanaume mwoga kwani alitoroka na kujificha ndani ya choo wakati majambazi walipowavamia na kumwaacha mkewe peke yake akiburuzwa na wahuni hao.

Jarida moja lilinukuliwa kwamba aliambia mahakama kuwa, "Mheshimiwa, bado sijapata nafuu kutokana na mshtuko niliopata wakati genge la wezi liliposababisha ghasia nyumbani kwetu. Yeye (mume) alijificha kwenye choo; akiniacha nikiteswa mbele ya wale majambazi ambao waliwatia hofu wakazi wote wa nyumba yetu. Mheshimiwa, wezi hao walipofika mwendo wa saa saba usiki mkuu, mume wangu hakupatikana kuwatetea watoto na mimi. Alijificha chooni. Alitoka wakiwa wamekwenda na anataka tuendelee kuishi katika nyumba hiyo.”

Mumewe kwa jina Abidemi alijitetea kwa kusema kwamba mkewe alikuwa na nia mbaya, ila akakiri kwamba alijificha ndani ya choo wezi walipoivamia nyumba yao.

“Ni kweli nilijificha chooni wakati majambazi waliokuwa na silaha walipovamia nyumba yetu. Jitihada zote nilizofanya za kumrudisha nyumbani zilishindikana kwa sababu alisema alikuwa na woga usio wa lazima.”

Inasemekana kuwa mwanamke huyo pia alimtuhumu mumewe kwa kuwa mchepuko na wanawake wengi na kuiomba mahakama kumzuia kutopewa haki ya kulea watoto baada ya talaka hiyo.

Mahakama iliamuru watoto wabaki chini ya ulezi wa mama huku ikimtaka mwanaume kuendelea kushughulikia watoto kwa kushirikiana na mkewe kwa amani na ustawi.