(+video) Rais Mteule Ruto akizungumza Sheng "Hawawezi Kutushinda Kang Kang"

Video imeibuliwa mitandaoni Ruto akisema kwa lugha ya Sheng kwamba washindani wake hawangeweza kumshinda.

Muhtasari

• “Mboka na Ruto ni mboka, unaona wanaogopa, hawawezi kutushinda kang kang,” Ruto anaonekana akisema nyuma ya hao vijana.

Video ya rais mteule William Ruto akizungumza lugha ya mtaani almaarufu Sheng kwamba washindani wa mrengo wake hawangeweza kumshinda imeibuliwa mitandaoni.

Katika video hiyo iliyopakiwa kwenye mtandao wa TikTok, Ruto anaonekana akiwa na kundi la vijana wa mtaani, ilipakiwa na mkuza maudhui Pitah Scarlet, rais Ruto anatabasamu kwa furaha huku hao vijana wengi wakizungumza na yeye kwamba hawezi kushindwa na kumalizia kwa maneno ya sheng.

“Mboka na Ruto ni mboka, unaona wanaogopa, hawawezi kutushinda kang kang,” Ruto anaonekana akisema nyuma ya hao vijana.

“Kumbe tulikuwa tumebashiri kweli bwana rais tukisema (hawawezi kutushinda The 5th). Utabiri wetu mzuri sasa umekuwa, ukweli hatimaye tunamshukuru Mungu,” Scarlet alifuatisha maneno hayo kwenye video hiyo.

William Ruto kipindi cha kampeni zake alionekana akitangamana na makundi mbali mbali ya watu haswa wale wenye maisha ya kadri katika kile alichokuwa akisema ni manifesto yake ya kuinua watu wa chini kupitia mpango wake wa kuboresha uchumi wa Bottom Up.

Jumatatu wiki hii, mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC Wafula Chebukati alimtangaza Ruto kuwa rais mteule wa Kenya kwa kura zaidi ya milioni 7 ambapo alimbwaga mwanasiasa mkongwe Raila Odinga ambaye alikuwa mshindani wake mkuu katika kinyang’anyiro hicho.

Ruto aliweka rekodi na kuwa naibu wa rais wa kwanza nchini Kenya kuwania urais na kushinda kwa mkondo wa kwanza huku akimshinda Odinga ambaye alikuwa anafanya jaribio lake la tano katika mbio za kuelekea ikulu ila akaoneshwa kivumbi tena.