Akothee awatahadharisha wanaume dhidi ya kumtongoza mitandaoni

Mama huyo wa watoto watano amewka wazi kuwa anapendelea kukutana na mtu ana kwa ana.

Muhtasari

•Akothee ameweka wazi kuwa hawezi  kuanguka kwenye mtego wa mapenzi ya mitandaoni kwa kuwa anapendelea kukutana na mtu ana kwa ana.

•Kutokana na uwongo mwingi kwenye mitandao ya kijamii, Akothee amewaonya watoto wake dhidi ya kutangamana na watu mtandaoni.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee amewataka wanaume kujiepusha kumtumia  jumbe tamu za kimahaba kwenye mitandao kwa nia kumtongoza.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, mama huyo wa watoto watano ameweka wazi kuwa hawezi  kuanguka kwenye mtego wa mapenzi ya mitandaoni kwa kuwa anapendelea kukutana na mtu ana kwa ana.

"Nashangaa jinsi watu wanavyopata mapenzi kwa kuchumbiana mtandaoni , nashangaa ningewezaje kuteleza kwenye Dm ya mtu na kutarajia itokee🤔, ninaogopa sana wanaume wanaoandamana na kulamba midomo yao 24/7. Ninapendelea kukutana na mtu wangu katika maisha halisi na mduara ambapo ninaweza kufuatilia historia yake. Unaweza hata kukutana na kifo chako kwa jina la mapenzi," Akothee alisema.

Mwimbaji huyo amedokeza kuwa hofu yake ya mambo ya mitandaoni imetokana na matukio ya nyuma yaliyoishia kuuvunja moyo wake.

Amedai kuwa yeye ni mwathiriwa wa unafiki ulio kwenye mitandao ya kijamii kwani amewahi kukutana na watu wengi bandia pale.

"Na moyo wangu mjinga, nimeamini maneno ya mashabiki, wengine walinasa moyo wangu na nikaamua kuwasaidia, ikawa deni. Niliwaalika wengine kwa likizo na wakageuka kuwa wa kunichukia, wengine waliomba kukutana nami na kutangaza jinsi wanavyonipenda, ili tu kuzima ubaya wao na kunigeuza kuwa mwathirika wa sumu yao," Akothee alifunguka.

Kutokana na uwongo mwingi kwenye mitandao ya kijamii, Akothee amewaonya watoto wake dhidi ya kutangamana na watu mtandaoni.

"Acha hata kuchumbiana, hata kuwa marafiki tu!" Alisema.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 42 ana watoto watano ambao wote wana kurasa za mitandao ya kijamii.

Binti zake watatu ni wakubwa na inaaminika kuwa wanasimamia akaunti zao wenyewe ilhali wanawe wawili ni wadogo na haijulikani wazi ni nani anayesimamia akaunti zao.