Mtu asiyeshugulikia mamake ni uchafu uliotolewa tumboni- Mamake Zuchu asema

Khadija Kopa amewakashifu wanaowatelekeza wazazi wao baada ya kufikia hatua ya kujisimama wenyewe.

Muhtasari

•Kopa amesema watu wanapaswa kuwasaidia wazazi wao kila wanapokumbwa na matatizo  bila ya kuzingatia uwezo wao wa kifedha.

•Mamake Zuchu alikumbana na ukosoaji mkubwa aliposema "Kuna wazazi wanazaa na kuna wengine wanakunya."

Khadija Kopa na binti yake Zuchu
Image: HISANI

Mwimbaji mkongwe wa taarab Khadjia Kopa amewakashifu wanaowatelekeza wazazi wao baada ya kufikia hatua ya kujisimama wenyewe.

Mama huyo wa malkia wa Bongo Zuhura Othman almaarufu Zuchu amesema watu wanapaswa kuwasaidia wazazi wao kila wanapokumbwa na matatizo  bila ya kuzingatia uwezo wao wa kifedha.

"Sio lazima mtoto afanikiwe. ,Mtoto ni mtoto, asiyefanikiwa na aliyefanikiwa. Lakini mtoto aliyezaliwa na mamake, hata kama hana kitu akisikia mamake ana tatizo anakimbia mbio. Hana uwezo wowote lakini atafika na kuuliza mamake kama amsongee ugali ama apike uji. Sio lazima akuje na kitu," Kopa alisema katika mahojiano na Mbengo TV.

Malkia huyo wa mipasho alikuwa akifafanua kuhusu kauli aliyotoa hapo awali "Kuna wazazi wanazaa na kuna wengine wanakunya."

"Tunao watoto wengine ambao wana uwezo, wakubwa, wana vyeo na pesa lakini baba zao wanahangaika. Hao ndio nikasema mama hakuzaa, kanyaa. Japo mtoto ana uwezo lakini hamshughuliki mzee wake. Mtoto yeyote asiyeshugulikia mamake hata kama hana kitu ni kama umetoa uchafu kwenye tumbo," Alisema.

Hapo awali, Kopa alikumbana na ukosoaji mkubwa aliposema "Kuna wazazi wanazaa na kuna wengine wanakunya."

Baadhi ya wanamitandao walidai kuwa  anawadhalilisha wazazi wengine kwa kuwa binti yake Zuchu kwa sasa ni msanii mkubwa. Mwanamuziki huyo mkongwe hata hivyo ameweka wazi kuwa hakukusudia kumdhalilisha yeyote.

Kopa ni mwimbaji taarab wa zamani mwenye kipaji kikubwa na ni wazi kuwa aliwatengenezea njia watoto wake. Zuchu, marehemu Omari Kopa na Black Kopa wote walijifunza na kujitosa kwenye usanii wa muziki.