"Alitaka tuoane nikakataa!" Baby Mama wa Ibraah afunguka sababu za kusitisha mahusiano yao

Clyna Sugar amesema hakuna maelewano kati yake na msanii huyo wa Konde Gang.

Muhtasari

•Sugar amedai kuwa uhusiano mbaya kati yake na Ibraah ulianza baada ya kukataa kujitosa kwenye ndoa naye.

•Sugar pia alimshtumu Ibraah kwa kuwa mwenye vurugu na kudai kuwa hata amewahi kumshambulia nusura amuumize.

•Amesema kuwa tangu drama hizo kujitokeza amekuwa akimpuuza msanii huyo  wa Konde Gang kwa kuwa aliona hafai kwake.

Clyna Sugar na Ibraah
Image: HISANI

Clyna Sugar, mlimbwende wa Bongo anayedai kuwa na mtoto na Ibraah amesema hakuna maelewano kati yake na msanii huyo wa Konde Gang.

Muuzaji vipondozi huyo amedai kuwa uhusiano mbaya kati yake na Ibraah ulianza baada ya kukataa kujitosa kwenye ndoa naye.

"Hatuna maelewano. Anahudumia mtoto anapojiskia. Yeye alitaka tuoane mimi nikakataa kwa hiyo akachukulia ni kama niko na mambo mengi. Ni kama yeye analipiza kisasi!" Sugar alisema katika mahojiano na Dizzim Online.

Kipusa huyo alisema licha ya kuwa na mtoto na Ibraah alikataa ndoa naye kwa kuwa aliona hawaendani. Hata hivyo aliweka wazi kuwa hatua ya kupata mtoto pamoja ni jambo ambalo tayari walikuwa wamekubaliana.

Alisema kuwa mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 24 aliona kama dharau wakati alipokata kuolewa naye.

"Mimi na yeye hatuendani kabisa. Sisi wawili tunakasirika haraka. Alafu tena ana wivu. Ni mwanaume fulani ambaye ukimfanyia kitu kinakuwa kama fimbo. Hasahau, ni mtu wa kulimbikiza sana vitu. Kitu kidogo anaweka," Alisema.

Sugar pia alimshtumu Ibraah kwa kuwa mwenye vurugu na kudai kuwa hata amewahi kumshambulia nusura amuumize.

Alisema mwanzoni alikuwa na uhusiano mzuri na Ibraah na hata alimhudumia katika kipindi chote cha ujauzito na kujifungua hadi wakati mtoto wao alipokuwa na umri wa miezi mitatu ambapo walianza kuvurutana.

Mnamo mwezi Mei, Sugar alijitosa kwenye mitandao kumwagiza msanii huyo kuwajibikia mtoto wao. Ibraah hata hivyo alionekana kukana kuwa na mtoto na mwanadada huyo. 

Kipusa huyo sasa amedai kuwa baadae Ibraah alimtafuta na kumuomba msamaha kupitia kwa bosi wake Harmonize.

"Mimi sikumtafuta. Alinipigia Harmonize. Tangu hicho kipindi alinipigia na kuniomba msamaha na kuniambia kuwa atapost kuonyesha Watanzania kuwa anataka kufanya DNA ili waelewe tulifanya vipimo na nikakubali," Alisema.

Sugar alisema tangu drama hizo kujitokeza amekuwa akimpuuza msanii huyo  wa Konde Gang kwa kuwa aliona hafai kwake.

"Silipizi kisasi, nimemuacha tu kwanza. Hakuomba DNA, hawezi kufanya DNA wakati anajua mtoto ni wake,

Licha ya mahusiano yao kugonga ukuta, Sugar amedai kuwa hana majuto yoyote kwa kuzaa mtoto na Ibraah.