Jina la Julius Kamau, jamaa anayejiita mwanaharakati na mtetezi wa haki za kibinadau si geni kwa Wakenya wengi.
Ni jamaa aliyejulikana kwa kuingia katika kumbi rasmi za taasisi za kiserikali na kuzua fujo huku akipinga baadhi ya taratibu kwa kile anasema ni kuwatetea wakenya.
Jumanne tena mwanaharakati huyo alifanya kile ambacho anazoea kufanya baada ya kufika katika mahakama ya upeo jijini Nairobi na kuzua fujo langoni huku akidai kwamba kesi inayopinga ushindi wa rais mteule William Ruto inafaa kutupiliwa mbali kwani haina maana yoyote kwa wakenya wanaoteseka kutokana na mfumuko wa uchumi.
Katika klipu ambayo ilipakiwa kwenye mitandao ya kijamii, mwanaharakati huyo alionekana akiteta vukali huku ameshikilia kwa nguvu chuma za lango la kuingia majengo ya mahakama hiyo na kupasa sauti kwamba kesi hiyo haina maana.
Kamau ambaye sasa wengi wanamjua kama mwanaharakati mwenye uzoefu wa kuzua fujo alisikika akipinga kwamba kesi hiyo hata ikienda upande wowote haitakuwa na tija kwa Mkenya mlala hoi.
Huku akiwa tumbo wazi, Kamau anasikika akiteta kwamba watu maskini wanateseka huku wanasiasa wakiteleza kwa utajiri.
"Hamwezi nishika kwa njia hii, ni hatia, ni hatia zaidi. Watu maskini wanateseka katika nchi hii, watu wanakufa huku wanasiasa wanataka kuteka nyara nchi yetu," anasikika akisema huku polisi wakipata wakati mgumu kumpoza.
Mwisho wa siku polisi walimmudu na kumbeba hobela hobela huku wakimchukua kusikojulikana.
Hii si mara ya kwanza kwa mwanaharakati huyo mwenye utata kuzua fujo kwani mwezi Juni tena alifurushwa katika mkutano wa IEBC na wagombea urais ambapo alielekea kuzua fujo.