DJ Mo na Size 8 wafichua jumba lao la kifahari wanalojenga licha ya masaibu ya ndoa

Size 8 alisema miaka tisa iliyopita aliomba kubarikiwa na nyumba yenye vyumba vitatu vya kulala.

Muhtasari

•Wanandoa hao waliutaja mradi huo kuwa 'matendo ya Bwana' na kufichua kwamba umekuwa ukiendelea kwa miezi mitatu unusu.

•Walisisitiza kuwa ni kweli walikuwa wameachana na kufutilia mbali madai kwamba ilikuwa njia ya kutafuta kiki tu. 

Image: INSTAGRAM// SIZE 8 REBORN

Mcheza santuri mashuhuri Samuel Muraya almaarufu DJ Mo na mkewe Size 8 wamefichua kuwa wanajenga nyumba ya kifahari.

Wawili hao walifichua jumba la ghorofa tatu wanalojenga katika video ambayo walichapisha kwenye akaunti yao ya YouTube.

Wanandoa hao waliutaja mradi huo kuwa 'matendo ya Bwana' na kufichua kwamba umekuwa ukiendelea kwa miezi mitatu unusu.

"Sio kwa nguvu zetu. Ni kwa mkono wa Mungu muweza yote," Size 8 alisema.

Wasanii hao wawili walikuwa wakizungumza huku wakiwa wamesimama mbele ya mjengo wao ambao haujakamilika. 

Size 8 alidokeza kuwa wakati walipokuwa wakifunga ndoa aliomba kubarikiwa na nyumba yenye vyumba vitatu vya kulala.

"Lakini angalia, Mungu anaweza kufanya zaidi ya yale ambayo unaweza kufikiria, kuomba au kutafakari," Alisema.

Kwa upande wake, DJ Mo alisema kuwa kwa muda wa miezi mitatu ambayo jengo hilo limekuwa likijengwa wamekuwa wakimtegemea Mungu kulifanikisha.

Wawili hao walifichua maendeleo ya nyumba yao wakati walipokuwa wakielezea hali halisi  ya ndoa yao ya miaka mingin iliyodaiwa kusambaratika.

Katika video waliyochapisha Jumatano, Size 8 ambaye kwa jina halisi ni Linet Munyali alithibitisha kwamba alikuwa amemuacha mumewe.

Mwimbaji huyo wa nyimbo za injili aliweka wazi kuwa alikuwa amegura ndoa yake  baada ya mumewe  DJ Mo kumkosea vibaya.

"Ndio nilitoroka. Nilikuwa nimemkasirikia sana DJ Mo. Alinikosea. Nilihitaji tu nafasi yangu niweze kupumua na kuongea na Mungu kwa kuwa naamini nikiwa na hasira na tuko kwa nyumba moja tutaongeleshana vibaya na kufanyiana vibaya," Size 8 alisema huku akiwa amesimama sako kwa bako na mumewe.

Alidokeza kuwa kosa ambalo DJ Mo alimtendea hadi kufanya atoroke ni kubwa, jambo ambalo mcheza santuri huyo alikiri.

"Ndio nilikosea, na nilisema pole," Mo alisema

Wawili hao walifichua kuwa watumishi wa Mungu na watu wengine wa karibu waliwasaidia kupatana na kusuluhisha mzozo wao.

"Tulifikia hitimisho na ufahamu wa kibiblia na sasa tumepatanishwa tena kwenye ndoa kwa sababu ya neema na rehema za Mungu," Size 8 alisema.

Aidha walisisitiza kuwa ni kweli walikuwa wameachana na kufutilia mbali madai kwamba ilikuwa njia ya kutafuta kiki tu.