(+video) Mchungaji awachapa viboko waumini kama njia ya 'kuwabariki'

Hakuna hata mmoja wao aliyeachwa, wadogo kwa mzee, mwanamume au mwanamke.

Muhtasari

• “Adhabu ya viboko iliacha shule na kwenda makanisani. Ninaona sera inakuja,” mmoja aliandika.

Wengi wanasema katika usasa huu wa utandawazi, ni vigumu kuficha maovu kwani kwa urais wa kamera, yanatumbuliwa tu kama majipu.

Nchini Uganda mchungaji mmoja amejipata matatani baada ya video kupakiwa kwenye mitandao ya kijamii ikifichua mbinu zake dhalimu za kuwapa baraka waumini kanisani.

Mchungaji huyo alinaswa kwenye kamera akiwapiga viboko waumini kanisani; wake kwa waume, wadogo kwa wakubwa huku akidai kwamba ni moja kati ya njia za kuwamiminia baraka na upako utokao wa bwana Mungu.

Katika video hiyo, mchungaji huyo aliyetambulika kwa jina Nabii Kevin Kintu anaonekana akiwaombea wafuasi wake alipowaomba waje kupokea fimbo hiyo ikiwa ni sehemu ya maombi hayo. Wafuasi walianza kukusanyika mbele ya kanisa, ambapo walipigwa migongo na makalio.

Mkanda huo wa video haukuwafurahisha wanamitandao waliouona kwani wengi walikashfu kitendo hicho, haswa pale ambapo nabii Kintu alikuwa habagui mtu hata mmoja mpaka wazee wa umri uliopitiliza ambao walilazimika kukubali ‘baraka’ ya nabii.

Wengine walisema kwamba adhabu ya kuchapwa viboko ilihama shuleni na sasa imekita mizizi makanisani ambapo waumini wote wanakipata cha mtema kuni wakiamini ni baraka na upako.

“Adhabu ya viboko iliacha shule na kwenda makanisani. Ninaona sera inakuja,” mmoja aliandika.

“Kitendo hiki kimekuwa kikifanywa nchini Uganda kwa muda mrefu sana na wale wanaoitwa "wachungaji, manabii na watu wa mungu". Lakini ni upuuzi kabisa kwamba vyombo vya habari vimekuwa vikiifunika.Serikali Ingilie Kati,” mwingine aliandika kwa ghadhabu.