Msanii Dufla anyoa rasta katika juhudi za kumtongoza Arnelisa Muigai

Mwimbaji huyo wa Dancehall aliweka wazi kuwa yupo tayari kulipa mahari kwa ajili ya Anerlisa.

Muhtasari

•Dufla alidokeza kuwa nywele fupi ni mojawapo ya mambo yanayozingatiwa na binti huyo wa seneta Tabitha Karanja kwa mwanamume.

•Mwimbaji huyo alikiri kwamba amekuwa akimchambua mrithi huyo wa Keroche kwa kipindi cha miaka mingi.

Anerlisa Muigai, Dufla Diligon
Image: INSTAGRAM

Mwanamuziki Dufla Diligon amenyoa rasta zake katika juhudi za kuthibitisha upendo wake kwa mfanyibiashara Anerlisa Muigai.

Katika chapisho alilochapisha kwenye Instagram, mwimbaji huyo wa dancehall alidokeza kuwa nywele fupi ni mojawapo ya mambo yanayozingatiwa na binti huyo wa seneta Tabitha Karanja kwa mwanamume.

"Sheria ya kwanza, ilibidi nifuate @anerlisa, ni nini kingine unataka nibadilishe?" Dufla aliandika chini ya video aliyopakia Instagram ambayo inayomuonyesha akiwa katika duka kinyozi akinyolewa nywele zake.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya mwanamuziki huyo kukiri upendo wake kwa mpenzi huyo wa zamani wa Ben Pol.

Katika kipindi chake cha 'Off Radar' kwenye Podcast, Dufla aliweka wazi kuwa yupo tayari kulipa mahari kwa ajili ya Anerlisa.

"Nataka nipeleke ng'ombe huko kwa Keroche. Nimejipanga kabisa. Mtu ni mimi pekee yangu, hizo zingine ni hekaya," Alisema.

Mwimbaji huyo alikiri kwamba amekuwa akimchambua mrithi huyo wa Keroche kwa kipindi cha miaka mingi.

"Mwanamke pekee ninayetaka katika maisha yangu sasa ni Anerlisa Muigai," Dufla alisema katika mazungumzo na KRG.

Katika chapisho lake lingine, mwimbaji huyo wa kibao 'Tempo' alifichua mazungumzo yake  ya simu na mzee kutoka kijiji chake  ambaye aliahidi kutoa ng'ombe watano kwa ajili ya mahari ya Anerlisa.

"Wazee wamebariki hii maneno, ng'ombe wanazidi kuongezeka. Ashe oleng ntauwo. Kibarua kinaanza," Alisema chini ya video hiyo ya mazungumzo.

Haya yanajiri wakati Anerlisa anaaminika kuwa kwenye mahusiano na mwanaume aliyetambulishwa kama Melvin Ibrahim.

Miezi kadhaa iliyopita mridhi huyo wa Keroche alifichua kuwa alijitosa kwenye mahusiano na Melvin miezi miwili tu baada ya kutengana na Ben Pol.

Mwaka wa 2020, Anerlisa na Ben Pol walifunga pingu za maisha ila wakatengana takriban mwaka mmoja baadae.