Huenda malkia wa muziki wa Bongo Zuhura Othman almaarufu Zuchu yuko 'sokoni' tena akitafuta mpenzi.
Katika chapisho lake la hivi punde, msanii huyo wa WCB amedokeza kwamba kwa sasa hayuko kwenye mahusiano.
"Single 😏 tena," Aliandika kwenye akaunti yake ya Snapchat.
Binti huyo wa Khadija Kopa aliambatanisha ujumbe wake na kipande cha shairi ya winner 'Ooh God look at me.'
Haya yanajiri hata kabla ya mashabiki kuweza kutatua kitendawili cha iwapo kwa kweli anachumbiana na bosi wake Diamond Platnumz.
Katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, wasanii hao wamedaiwa kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi huku ukaribu wao na vitendo vyao vya kutiliwa shaka pamoja vikionekana kuziunga mkono tetesi hizo.
Mara nyingi wawili hao wameonekana wakistarehe pamoja, wakijivinjari pamoja, wakicheza miondoko ya kimahaba jukwaani, wakisema maneno ya kimahaba kuhusu kila mmoja, kukumbatiana na hata kubusu.
Hata hivyo, hawajawahi kutangaza mahusiano yao wazi wala kuukana. Wamekuwa wakiwazungusha mashabiki wao na kuwaacha kubahatisha tu.
Mwezi Februari, mashabiki walisubiri kwa hamu na ghamu harusi kati ya wawili hao ambayo ilikuwa imedaiwa kufanyika mnamo siku ya Valentines.
Hata hivyo, siku hiyo ilipofika harusi hiyo haikufanyika huku wasanii hao wakibainisha kuwa wote wapo kwenye mahusiano mengine.
"Niko kwenye mahusiano. Nina furaha. Nafurahia, mahusiano yangu yananipa raha na amani. Huba limetaradadi, mahaba ndi ndi ndi" Diamond alisema katika mahojiano na Wasafi Media mnamo usiku wa Valentines.
Takriban miezi miwili iliyopita, Diamond kwa mara ya kwanza alijitambulisha hadharani kama mume wa msanii huyo wake.
"Huyo ni mume wa Zuuh," Bosi huyo wa WCB aliandika chini ya video iliyoonyesha akiwa jukwaani ambayo ilipakiwa kwenye Instagram.
Siku chache baadae hata hivyo Zuchu akizungumza na mtangazaji wa Wasafi Media Ankali Mambi alionekana kuukana ujumbe huo.
Malkia huyo wa Bongo alidai kuwa hakuona comment hilo la bosi wake na hata kuzua shaka ikiwa kwa kweli ni yeye alitajwa.
"Zuuh wako wengi. Ni kweli naitwa Zuuh lakini si Zuuh mimi, kama ingekuwa mimi angeniambia. Itakuwa Zuuh mwingine," Zuchu alisema.
Zuuh ni jina la utani la staa huyo kutoka Zanzibar.
Katika mahojiano hayo, binti huyo wa Khadija Kopa bado alisisitiza kuwa uhusiano wake na Diamond ni wa kikazi.