Staa wa Bongo Harmonize anaonekana kuridhishwa sana na hatua alizochukua kurudiana na mchumba wake Frida Kajala Masanja.
Miezi kadhaa iliyopita, Bosi huyo wa Konde Music Worldwide alitangaza kutengana na mpenzi wake kutoka Australia, Brian Jai na kukiri kuwa moyo wake bado alimtamani Kajala ambaye aliachana naye Aprili mwaka jana.
"Kuhusu Briana, sina Tatizo naye kabisa, yeye ni mtu mzuri ila hatuko pamoja, sababu moja nilimwambia nimetengana na mtu bila kugomabana na nampenda sana. Sasa sina uhakika kama nimemove on, lolote linaweza kutokea maana itakuwa ni kitendo kizalendo pia mimi kurudi nyumbani," alisema mwezi Machi.
Mara baada ya tangazo hilo, Harmonize alianza hatua za kurejesha mahusiano yake na Kajala huku akifanya juhudi kumuomba msamaha hadharani na kumnunulia zawadi kemkem katika juhudi za kumshawishi kurudi.
Hatimaye juhudi za mwimbaji huyo zilizaa matunda kwani wawili hao walirudiana mwezi Mei. Mwezi mmoja baadae Harmonize alimvisha mpenzi huyo wake pete ya uchumba na kudokeza harusi hivi.
"Ndoto yangu ilikuwa kuwa na urafiki wa muda mrefu na ikiwezekana urafiki ambao ungedumu milele na mpenzi wangu Frida na nimekuwa nikimwambia hilo karibu kila siku," Harmonize alisema baada ya muigizaji huyo kukubali ombi lake la ndoa.
Kajala kwa upande wake alisema, ""Rajab nitakupenda leo, kesho hadi milele,"
Tangu kurudiana kwao wapenzi hao wawili wamepiga hatua kubwa pamoja, jambo ambalo Konde Boy amebainisha.
Mwimbaji huyo sasa amewashauri wapenzi kukumbatia mazungumzo ya kina na kuomba msamaha kila wanapotofautiana huku akibainisha kuwa hatua hizo zinaweza kurekebisha mambo mengi.
'Mazungumzo moja ya kina na kuomba msamaha yanaweza kurekebisha mengi. Anza sasa, hujachelewa," Harmonize alishauri kupitia ukurasa wake wa Instagram.
Aliambatanisha ujumbe huo wake na picha zinazoonyesha akijivinjari na mchumba huyo wake kwenye bwawa la kuogelea.
Mwanzilishi huyo wa Kondegang alimtambua Kajala sio kama mkewe tu bali pia kama bosi wake.