(+screengrab) Mwanamke avujisha meseji za mwanaume akimtongoza

Mwanamke huyo alishangazwa na mwanaume huyo kugonga msumari juu ya kichwa moja kwa moja bila kupita kando kando.

Muhtasari

• “Badala ya kupitia kando kando kama kikohozi kinachojaribu kuja na hakiji, acha niweke bayana kabisa… nataka tuwe marafiki wa ‘mpaka kifo kitutenganishe"

Mwanamke apakia mazungumzo ya mwanaume aliyekuwa anajaribu kumtongoza
Mwanamke apakia mazungumzo ya mwanaume aliyekuwa anajaribu kumtongoza
Image: LOHWIS//TWITTER

Lohwis, Mwanamke mmoja ambaye kulingana na utambulisho wake kwenye mtandao wa Twitter ni mwandishi katika jarida la New York Times amezua gumzo kali katika mtandao huo baada ya kupakia picha ya mazungumzo ya mwanaume ambaye alikuwa anajaribu bahati katika kumtongoza.

Akitetea hatua yake ya kuvujisha meseji za faragha amabzo mwanaume huyo alimwandikia nyingi hata bila kusubiri mwanadada ajibu, Lohwis alijitetea kwamba kufanya hivo hakulenga kumkosea heshima wala kumdhihaki bali ni kwa sababu alivunjwa mbavu na jinsi mwanaume huyo alimrushia mistari moja kwa moja pasi na kupita kando kando ya mada husika.

Katika meseji hizo kadhaa, mwanaume alianza moja kwa moja kwa kusema kwamba hana muda wa kupita kando kando na badala yake kugonga msumari juu ya kichwa kwamba anamtaka kimapenzi na hata akimkataa hana chochote cha kupoteza.

“Sina nguvu ya kupita kando kando, mimi nakupenda na ningependa tuwe marafiki. Si tu marafiki wa salamu bali urafiki ambao unaeza endelea kwa mambo yenye umuhimu mkubwa,” mwanaume huyo alichomoa risasi pasi na kusita, moja kwa moja.

Aliendelea kujieleza kwenye msururu wa meseji kwamba angependa wawe marafiki wa ukaribu kabisa hata kuambizana fikira na mawazo ya kibiashara, kulishana Imani ya rooni na pia urafiki wa kuishi pamoja kama wapenzi.

Alipoona hajajieleza kwa lugha ya kueleweka, alijirekebisha kwa meseji nyingine kwamba anataka waishi kwa kaule ile ya kanisani wakati wa kufunga ndoa – mpaka umauti ututenganishe!

“Badala ya kupitia kando kando kama kikohozi kinachojaribu kuja na hakiji, acha niweke bayana kabisa… nataka tuwe marafiki wa ‘mpaka kifo kitutenganishe. Kuna kitu lazima kiuwe mwanaume nami ni bora nife nikifuata takwa la Moyo wangu kuliko kufuata njia ndefu” Mwanaume alitema nyongo.

Mwanadada huyo kwa kuonesha mshangao wake, alipakia meseji hizo na kusema amesogezwa sana na ujasiri wa mwanaume huyo na angependa kukutana na yeye ila akasisitiza kwamba hawezi kuahidi chochote kitakachotokea mbele ya safari.

“Kuchapisha hii sio kumdhihaki mtumaji. Kinyume chake, hii imenifanya nicheke sana. Ninapenda nguvu na ujasiri. Ninatarajia kabisa kujihusisha naye. Siahidi chochote. Nilitaka tu kusema wanaume wanajua wanachotaka, ikiwa sio wewe, sivyo!” Lohwis alimaliza kwa ushauri kwa kina dada.