Sonnie, Mulamwah watofautiana kuhusu kuhusishwa kwa binti yao katika kutengeneza pesa

Muigizaji huyo alisema anafanya hilo katika juhudi za kurahisisha maisha yake na bintiye.

Muhtasari

•Sonnie amesisitiza kuwa Keilah Oyando ni chapa na kubainisha kuwa  hapati faida yoyote kutokana na ridhaa  anazopata bintiye.

•Mulamwah alimshtumu mzazi huyo mwenzake kwa kumtumia binti yao kama kifaa cha kutengeneza pesa na kumsihi akome.

Carrol Sonnie na aliyekuwa mpenzi wake Mulamwah
Image: HISANI

Tofauti kati ya wapenzi wa zamani Mulamwah na Carrol Sonnie zimeendelea kushika kasi huku  sasa wakitofautiana kuhusu jinsi binti yao anavyoshughulikiwa. 

Sonnie ambaye ndiye anayeishi na mtoto huyo wa mwaka mmoja kwa sasa baada ya kutengana na Mulamwah mwaka jana ameeleza kutoridhishwa kwake na madai ya mchekeshaji huyo kuwa anamtumia binti yao kujitengezea pesa.

Muigizaji huyo amesisitiza kuwa Keilah Oyando ni chapa na kubainisha kuwa  hapati faida yoyote kutokana na ridhaa  anazopata bintiye.

"Keilah anahitaji pesa, Keilah anahitaji diapers, tunahitaji pesa jamani na ni lazima tuzitafute, pesa  zote ni zake sio zangu. Hiyo pesa hata hainisaidii, ni ya mtoto," alisema katika mahojiano na Nicholas Kioko.

Sonnie aliweka wazi kuwa mikataba yote ya uidhinishaji ambayo anasaini kwa ajili ya bintiye ni katika juhudi za kurahisisha maisha yao.

"Lazima tutafute unga. Lazima nitafutie mtoto wangu unga. Mimi na mtoto wangu tunajaribu kuangalia jinsi tutafika mahali tusihangaike.  Sidhani namtumia mtoto wangu. Ni mtoto wangu, ni binti yangu!" alisema

Huku akimtakia Keilah heri ya siku ya kuzaliwa mnamo Jumamosi, Mulamwah alidokeza kuwa haijakuwa rahisi kushirikiana na Sonnie katika malezi.

Mchekeshaji huyo alimshtumu mzazi huyo mwenzake kwa kumtumia binti yao kama kifaa cha kutengeneza pesa na kumsihi akome.

"Tusimtumie mtoto kama chambo ili kupata likes kwenye mitandao ya kijamii kupenda mitandao ya kijamii, uthibitisho na kupata faida ya pesa. Mtoi sio kazi," Mulamwah alimwambia aliyekuwa mpenziwe.

Mchekeshaji huyo hata hivyo hakukosa kutambua juhudi za Bi Sonnie katika malezi ya binti yao na kumpongeza kwa hilo. 

Sonnie pia alipuuzilia mbali madai kuwa amekuwa akimzuia Mulamwah kumuona binti yao na kufanya uzazi wenza kuwa ngumu.

"Mimi sijawahi kukataza mtu kuja kuona mtoto wake. Sina mengi ya kuzungumzia maneno hayo," alisema.

Wakati akimsherehekea bintiye mnamo siku ya kuzaliwa, muigizaji huyo  alibainisha kuwa ni furaha kubwa kwake kumuona akikua.

"Kukuona ukikua kila siku imekuwa nyakati zangu bora zaidi. Kwa kweli siwezi kungoja kukuona ukizeeka na kuwa Mtoto anayemcha Mungu.. Ninakupenda sana. Heri ya kuzaliwa mpenzi wangu," alisema.

Keilah ambaye alizaliwa katika kipindi ambacho wazazi wake walikuwa wakitengana alitimiza mwaka mmoja Jumamosi.