Zari kufunga ndoa hivi karibuni baada ya mpenzi wake mdogo kulipa mahari

Mwanasoshalaiti huyo amefichua kuwa mpenziwe anapanga kupeleka posa kwa baba yake nchini Uganda.

Muhtasari

•Zari amedokeza kufunga pingu za maisha na Shakib Cham  baada ya kufichua kuwa mpenziwe huyo anapanga kupeleka posa kwa baba yake.

•Zari aliwatupia vijembe wakosoaji wa mahusiano yake na Bw Shakib huku akiwathibitishia kuwa juhudi zao kuwatenganisha zilikuwa zimefeli.

Shakib Cham na mpenziwe Zari Hassan
Image: INSTAGRAM// SHAKIB CHAM

Ni wazi kuwa mwanasoshalaiti Zari Hassan anayafurahia sana mahusiano yake mapya na hivi karibuni huenda tukashuhudia akifunga ndoa.

Mpenzi huyo wa zamani wa Diamond Platnumz amedokeza kufunga pingu za maisha na Bw Shakib Cham Lutaaya baada ya kufichua kuwa mpenzi huyo wake wa sasa anapanga kupeleka posa kwa baba yake nchini Uganda.

"Shakib aliniambia jana kuwa anataka kukutana na baba yangu. Anataka kutoa posa kwa ajili ya ndoa, yuko tayari kunioa," Zari alisema kwa Kiganda  katika video ambayo ilipakiwa kwenye mtandao wa Snapchat.

Katika video hiyo fupi, mama huyo wa watoto watano aliendelea kuwatupia vijembe wakosoaji wa mahusiano yake na Bw Shakib huku akiwathibitishia kuwa juhudi zao kuwatenganisha zilikuwa zimefeli.

"Waliosema itaishia kwa machozi rudini kwa waganga wenu mkaombe warudishe hela, uchawi haukufanya kazi," alisema.

Hivi majuzi Zari alibainisha kuwa mpenzi wake mpya amemletea amani ambayo imemwezesha kukua na kung'aa zaidi.

"Nanza kuwa mkubwa. Naona shavu. Nimejipa amani sana. Bwana Lutaaya unanipa amani sana  kwa maana, watu, ngojeni niwaambie kuhusu amani ya  akili, hiyo nawaambia hata ufanye nini, unakua mkubwa zaidi hata usipokula," alisema kupitia Tiktok.

Mwanasoshalaiti huyo alimtaka Shakib kuendelea kumpatia mahaba anayompa na kumbainishia kuwa yanafanya kazi.

"Bwana Lutaaya chochote unachofanya, ongeza zaidi. Niongezee dozi nyingine, chochote unachofanya kwa sababu zinafanya kazi, zinafanya kazi. Hata hao wanaoroga wamekata tamaa, wanahitaji kurejeshewa pesa zao. Bado nina amani, nendeni mkaombe kurejeshewe pesa zenu," alisema.

Zari amekuwa akitetea mahusiano yake na Lutaaya hasa kwa kuwa amekosolewa sana kufuatia utofauti wao wa kiumri.

Wiki chache zilizopita alifichua kuwa amempiku mpenzi huyo wake  kwa takriban miaka kumi.

"Mpenzi wangu sio mdogo. Ana miaka 30 anaelekea 31 Desemba mwaka huu. Yeye sio mdogo, anakaa mdogo. Mimi natimiza miaka 42 mwaka huu na huwezi kujua," Alisema.