DJ Creme amsherehekea mkewe licha ya kusema ndoa ni utapeli hapo awali

Wanandoa hao wawili wamekuwa kwenye ndoa kwa miaka 14 .

Muhtasari

•Dj Creme amesherehekea ndoa yake na mke wake Denise Kingang'i.

•Creme na mkewe wamebarikiwa na watoto wawili, mvulana anayeitwa Jamari na msichana waliyemwita Zawadi.

DJ Creme na Mkewe
Image: HISANI

Mcheza santuri George Njuguna alimaarufu Dj Creme amesherehekea ndoa yake na mke wake Denise Kingang'i.

Wanandoa hao wawili wamekuwa kwenye ndoa kwa miaka 14 .

“Wueh, Mungu wangu anaweza, nimepata hii kwa picha za hapo awali. Muda kweli unakimbia,” Creme aliandika chini ya picha ya kumbukumbu iliyomuonyesha akiwa na mkewe katika siku za nyuma.

Wanamitandao waiwapongeza Creme na mkewe huku baadhi wakizungumzia maendeleo ya ndoa yao.

Creme na mkewe wamebarikiwa na watoto wawili, mvulana anayeitwa Jamari na msichana waliyemwita Zawadi.

Ijapokuwa ndoa yao imekuwa na misukosuko kama ndoa yoyote ile, wawili hawa wameweza kutatua shida zozote kwa pamoja.

Hapo awali Creme aliwahi kusema kuwa ndoa ni ulaghai, maneno ambayo hayakuwafurahisha wengi akiwemo mkewe Denise.

Baadaye katika mahojiano, DJ Crème alikiri kwamba anajuta kulaani ndoa na kumfanya mkewe kuangaziwa na kukosolewa na umma.

“Baada ya muda niligundua kuwa nimefanya kosa kubwa, hasa kusema Ndoa ni utapeli. Hizo zilikuwa ni hisia tu na ninajuta sana kwa sababu zimenigharimu vitu vingi. Je, unaweza kufikiria watoto wangu katika siku zijazo watakuja kunionyesha video ya YouTube wakisema Baba kwa nini ulisema ndoa ni ulaghai?” alisema.

Baada ya sakata hiyo Creme aliweza kutatua shida hiyo iliyoikumba ndoa yake na kuweza kumrudisha mkewe na watoto wake nyumbani.

DJ huyo alikiri kuwa kila ndoa ina misukosuko yake ila hakueleza jinsi walivyofaulu kujenga ndoa yao upya. 

"Familia inaendelea vizuri, wamerudi nyumbani na wametulia sasa. Mungu ni mwenye neema ya kutosha alirudisha familia na inashangaza,Siwezi hata kuelezea hisia,”alisema.

Baada ya hapo, Creme ameweza kuonyesha mahaba yaliyo kati yake na mkewe.

"Nakupenda kila siku," alisema mtandaoni mwezi wa Agosti tarehe 20.