'Wanaume wakubwa wananunua ndege wewe unanunua matatu'-Dimana Mkare amkejeli Willy Paul

Alisema kuwa Willy Paul ni msanii mkubwa na hafai kununua kitu kidogo kama matatu.

Muhtasari

• Diman alisema vijana wa mtaaani wangependa kujua asili ya mafanikio ya wanamuziki ama watu maarufu.

Mwanamitindo Diman Mkare amemtania Willy Paul kwa kununua matatu ila alimpongeza kwa  hatua hiyo.

“Wasanii wakubwa wananunua helikopta, wewe unanunua matatu,”alisema mwanamitindo huyo.

Aliongeza kuwa Willy Paul ni msanii mkubwa na hafai kununua kitu kidogo kama matatu.

Mwanamitindo huyo aliyejitambulisha kama mnyamwezi mwenye kitengo chake ama ‘odi’ wa shughuli alisema anatarajia msanii mkubwa kama Willy Paul  kuwatia moyo vijana wa mtaani.

Alisema kuwa vijana wa mtaaani wangependa kujua asili ya mafanikio ya wanamuziki ama watu maarufu.

Diman alisema kile kidogo ambacho wasanii wanapata kwenye kazi zao wakitumie vizuri wakifikiria maisha ya kesho. 

Hii ni baada ya Wilson Abubakar Radido alimaarufu Willy Paul kuzindua gari lake jipya lililokuwa limepambwa kwa njia ya kipekee.

Willy Paul alisema huenda hiyo ndio biashara atakayokuwa anafanya, kuyapamba magari na kisha kuyakodisha kwa matumizi maalum.

“Nimefanya biashara kadhaa na hii ya hivi sasa haijakuwa kwenye nyanja yangu ya muziki. Sasa nitaingia kwenye biashara ya matatu na kabla nijitolee kuifanya kabisa, tumeleta tatu hadi sasa,”alisema.

Wengi walijitokeza kumpongeza kwa hatua hiyo kubwa huku wengine wakisema wanamuziki wengine wajifunze kuwekeza katika biashara mbalimbali kama Willy Paul anavyofanya kwa wakati huu.

Aliweka wazi kwamba gari lake la kwanza alilozindua halitatumika kama matatu bali litakuwa la kusafirisha watu kwenye hafla mbalimbali.

Alisema atakayetaka kuikodisha  awasiliane na wasimamizi wake na atasaidiwa.