"Diamond alilipa mahari!" Lynn azungumzia ndoa yake fupi na Diamond, sababu ya kutengana

"Ukinicheat safari yako imeishia hapo. Mimi ni mtu mkweli sana," alisema.

Muhtasari

•Lynn ameweka wazi kuwa yeye na bosi huyo wa WCB walipendana sana katika kipindi cha mahusiano yao.

•Lynn amefichua kuwa aliondoka kwenye ndoa yake na Diamond baada ya staa huyo wa Bongo kuchepuka.

Official Lynn, Diamond Platnumz
Image: INSTAGRAM

Msanii wa Bongo Irene Louis almaarufu Official Lynn amefichua alikuwa kwenye ndoa na Diamond Platnumz kwa takriban mwaka mmoja unusu.

Wasanii hao wawili walichumbiana kwa muda hadi mwishoni mwa 2018 ambapo Diamond alimtema Lynn. Baadae staa huyo wa Bongo alijitosa kwenye mahusiano na mwanamuziki Tanasha Donna kutoka Kenya.

Lynn ameweka wazi kuwa yeye na bosi huyo wa WCB walipendana sana katika kipindi cha mahusiano yao.

"Kipindi ambacho nilikuwa na Diamond nilikuwa sijulikani. Watu walikuja kujua baadae wakati tushakuwa hadi watu wamekuja nyumbani na kufanya kila kitu," alisema katika mahojiano na Wasafi Media.

Kipusa huyo alifichua kuwa Diamond tayari alikuwa amewatuma wawakilishi kadhaa nyumbani kwao kwa ajili ya posa na mahari.

"Haikuwa nyepesi kama wengine," alisema.

Licha ya Diamond kupiga hatua nyingi muhimu za ndoa na Lynn kuwa tayari kufunga pingu za maisha naye, mahusiano yao hata hivyo hayakufika hata mwaka wa pili.

Lynn amefichua kuwa aliondoka kwenye ndoa yake na Diamond baada ya staa huyo wa Bongo kuchepuka.

"Ukinicheat safari yako imeishia hapo. Mimi ni mtu mkweli sana," alisema.

Mlimbwende huyo alisema kuwa hawezi kumzuia mume wake kutoka nje ya ndoa lakini hawezi kuendelea nayo pindi akigundua.

Hapo awali Lynn aliwahi kufichua kuwa alikutana na Diamond kwa mara ya kwanza wakati wakirekodi video ya Rayvanny.

Pia aliwahi kufichua kuwa alibeba ujauzito wa mwanamuziki huyo ila akaupoteza ukiwa na miezi wa tatu.

"Nilikuwa tayari mjamzito lakini niliipoteza katika mwezi wa tatu. Sijui kwa nini nilipoteza mimba hiyo, labda ulikuwa ni mpango wa Mungu, " alisema katika mahojiano ya awali na Wasafi Media.

Kando na Diamond, Lynn aliwahi kuwa kwenye mahusiano na mwimbaji wa RnB kutoka Bongo, Tommy Flavour.