Mke wa zamani wa Harmonize, Sarah Michelotti akwenda mahakamani kutaka talaka

Wawili hao walikuwa kwenye ndoa kwa takriban miaka minne.

Muhtasari

•Sarah ambaye alitengana na Harmonize takriban miaka mitatu iliyopita anaripotiwa kufika mahakamani kufuatilia madai ya talaka yao.

•Kumekuwa na tetesi kuwaSarah  anakusudia kuvichukua vitu  vyote alivyompa Harmonize.

Harmonize na aliyekuwa mpenzi wake Sarah Michelloti
Image: HISANI

Leo hii, Septemba 27, aliyekuwa mke wa Harmonize, Bi Sarah Michelotti anaripotiwa kufika mahakamani kwa ajili ya kesi ya talaka yake na mwimbaji huyo.

Video ambayo iliweza kufikia Radio Jambo ilimuonyesha mwanamitindo huyo kutoka Italia katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke huko Dar es Salaam, Tanzania huku akiwa ameandamana na baadhi ya wanafamilia wake.

Sarah ambaye alitengana na Harmonize takriban miaka mitatu iliyopita anaripotiwa kufika mahakamani kufuatilia madai ya talaka yao. Wawili hao walikuwa kwenye ndoa kwa takriban miaka minne.

Mwanamitindo huyo aliwasili nchini Tanzania mapema mwezi huu na siku za hivi majuzi  amekuwa akijivinjari huko  Zanzibar.

Katika kipindi cha siku kadhaa ambazo zimepita mwanamitindo huyo amekuwa akipakia picha zinazomuonyesha akifurahia muda wake katika kisiwa hicho  na kufichua kuwa yuko katika kijiji cha Kiwengwa.

"Najihisi nyumbani... Zanzibari," Sarah aliandika chini ya chapisho la wiki jana.

Mwanamitindo huyo amekuwa akitumia ziara yake ya Tanzania kurudisha kumbukumbu za kipindi ambacho aliishi pale na pia kukutana na baadhi ya marafiki wake ambao aliwapata wakati huo.

Hapo awali tetesi ziliibuka kuwa alikuwa ameandamana na kundi kubwa la wanasheria na anakusudia kuvichukua vyote alivyompa Harmonize. Inadaiwa baadhi ya mali ambayo bosi huyo wa Konde Music Worldwide anamiliki ikiwemo lebo, nyumba na magari kadhaa ni ya mpenzi huyo wake wa zamani.

Sarah alimtema Harmonize mwaka wa 2020 baada ya kuwa kwenye mahusiano naye kwa takriban miaka minne.Mwaka jana Harmonize alitunga wimbo 'sorry' kwa ajili ya kumuomba msamaha mpenzi huyo wake wa zamani.

Mwimbaji huyo alisema ndoa yao ilianza kusambaratika wakati mpenziwe alikuwa amesafiri kuenda kwao na baada ya kuwa pweke kwa muda akapata majaribu ya kutembea na mwanadada aliyemzalia mtoto

"Mimi nilikuwa Tanzania na kama unavyojua umbali wa mapenzi unapokuwa nikaishia kutembea na mwanamke ni mama Zuuh sasa hivi. Kwa mipango ya mwenyezi Mungu nikamfanya mjamzito. Akaniambia na kuniuliza ikiwa niko tayari ama atoe. Kwa kuwa mimi ni Muislamu, kuutoa mimba ni kushiriki dhambi. Sikuwa tayari kwa hayo. Niliamua ni njia ambayo mwenyez Mungu aliamua kunipitisha" Harmonize alisema.

Alisema kuwa Sarah aliumia sana moyoni baada ya kupata habari kwamba alikuwa amecheza karata nje na kupachika mwanadada mwingine ujauzito.

Alieleza kuwa  alijaribu sana kumshawishi mpenziwe amsamehe ili warejeshe mahusiano yao ila juhudi zake zote ziliangulia patupu.

"Ilimuumiza sana Sarah kwa sababu mnapokuwa na mtu kwenye mahusiano mnakuwa na ndoto za kupata familia bora. Ilimuumiza sana na akashindwa kukubali. Kwa kipindi kirefu nilikuwa nikificha  almaradi tu mahusiano yetu yaweze kuenda vyema. Nilikuwa naamini ingawa alikuwa na hasira wakati ungefika akubali matokeo. Nilikuwa natafuta njia zingine za kuenda kwake ili awe sawa na yote lakini kwa bahati mbaya ilishindikana hakuweza kukubali na akaenda"  alisimulia.