Muigizaji mashuhuri wa Bongo Wema Sepetu na mwanamuziki Whozu hatimaye wameyaweka wazi mahusiano yao.
Kwa muda mrefu wawili hao wamekuwa wakidaiwa kuwa wapenzi ila hawakuwahi kujitokeza hadharani kukiri hilo.
Siri ya mahusiano yao ilifichuka usiku wa kuamkia Jumatano wakati wa karamu ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya Wema. Leo hii, Septemba 28, mpenzi huyo wa zamani wa Diamond ametimiza miaka 32.
Wawili hao walionekana wakijivinjari pamoja, wakikumbatiana, kudensi pamoja na hata kubusu mbele ya kamera kabla ya Wema kueleza jinsi alivyozama kwenye mahaba anayopewa na mwimbaji huyo.
"Kwa muda mrefu nimekuwa sina raha. Nimekuwana huzuni, nimekuwa nikilia lakini tangu nilipokutana na Chibaba wangu nimekuwa na raha na amekuwa akiweka tabasamu kwenye uso wangu," alisema.
Muigizaji huyo alisema alifurahishwa sana na karamu ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ambayo aliandaliwa na mpenziwe. Maendeleo ya karamu hiyo yalipeperushwa moja kwa moja kwenye ukurasa wa Instagram wa Whozu.
Katika video hiyo ya moja kwa moja, Wema ambaye alionekana mlevi hakuficha hasira yake kwa waliokosoa mahusiano yake mapya.
"Eti wanasema Whozu hataki, angekuwa hataki angenifanyia hivi vyote!" aliwaambia wakosoaji wake.
Mpenzi huyo wa zamani wa Diamond Platnumz alibainisha kuwa furaha yake ndio kitu cha muhimu zaidi katika maisha yake, kitu ambacho Whozu ameweza kumpatia.
Wema na Diamond walichumbiana kwa muda hadi walipotengana mwaka wa 2014. Baadae Diamond alijitosa kwenye mahusiano na Zari.
Kando na Diamond, Wema amewahi kuchumbiana na wanaume wengine kadhaa akiwemo marehemu muigizaji Steven Kanumba.