Kajala aingilia kati talaka ya Harmonize, Sarah adaiwa kutaka wagawane mali

Mwimbaji huyo amesema aliondoka bila chochote walipoachana na Sarah.

Muhtasari

•Kwa sasa Sarah yupo nchini Tanzania kwa ajili ya muendeleo wa talaka yake na Harmonize, takriban miaka miwili baada yao kutengana.

Bosi huyo wa Kondegang ameshauriwa na mchumba wake Kajala asifadhaishwe na mpenziwe huyo wa zamani.

Kajala Masanja, Sarah Michelloti, Harmonize
Image: INSTAGRAM

Drama zimeendelea kutanda kati ya staa wa Bongo, Harmonize na aliyekuwa mpenzi wake wa muda mrefu Sarah Michelloti.

Kwa sasa Sarah yupo nchini Tanzania kwa ajili ya muendeleo wa talaka yake na Harmonize, takriban miaka miwili baada yao kutengana.

Imeibuka kuwa sasa Harmonize anapanga kuandika talaka tatu baada ya mwenzi huyo wake wa zamani kuwasilisha kesi mahakamani.

"Yani anashtaki kama mimi nimemuoa!"  Harmonize alimuandikia mchumba wake wa sasa muigizaji Kajala Masanja kwenye screenshot ya mazungumzo yao aliyochapisha kwenye Instastori zake.

Katika mazungumzo hayo, aliendelea kufichua kuwa sababu ya Sarah kudai talaka ni kwa kuwa anataka wagawane mali.

Hata hivyo alidokeza kuwa hakuna mali yoyote ambayo anapaswa kugawana na mwanamitindo huyo kutoka Italia huku akibainisha kuwa aliondoka bila chochote wakati walipoachana mwishoni mwa mwaka 2020.

"Tumeachana nikaanza kulala nyumbani kwako daah hata pa kulala nilikuwa sina. Hizo mali zilikuwa wapi jamani!! Daah," alimwandikia Kajala.

Bosi huyo wa Kondegang hata hivyo ameshauriwa na mchumba wake Kajala asifadhaishwe na mpenziwe huyo wa zamani.

"Achana naye," alimshauri.

Harmonize ambaye alionekana kufurahishwa na ushauri wa mchumba wake alisema,  "LOL, hata mke wangu hasumbuki. Kuwa na mwanamke mwenye akili haha!! Niko high tu, sijui mbona napost!"

Jumatano Bi Sarah  alifika katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke huko Dar es Salaam, kwa ajili ya kesi ya talaka yake na Harmonize.

Video iliyofikia Radio Jambo ilimuonyesha mwanamitindo huyo mahakamani akiwa ameandamana na baadhi ya wanafamilia wake

Sarah ambaye alitengana na Harmonize takriban miaka miwili iliyopita aliripotiwa kufika mahakamani kufuatilia madai ya talaka yao. Wawili hao walikuwa kwenye ndoa kwa takriban miaka minne.