Harmonize na Kajala wazika tetesi za matatizo katika mahusiano yao

Kajala alionekana mwenye bashasha wakati akimlaki mchumba wake nyumbani.

Muhtasari

•Alhamisi jioni mchumba wake Kajala Masanja alipakia video fupi iliyoonyesha wakikumbatiana baada yake kufika nyumbani.

•Tetesi hizo zilianza siku kadhaa baada ya wawili hao kuchapisha jumbe za kutia wasiwasi kwenye kurasa zao.

Wawili hao wamezika tetesi kuwa kuna matatizo kwenye mahusiano yao.
Harmonize na Kajala Wawili hao wamezika tetesi kuwa kuna matatizo kwenye mahusiano yao.
Image: INSTAGRAM// KAJALA MASANJA

Staa wa Bongo Harmonize hatimaye amerejea nyumbani Tanzania baada ya ziara ya siku kadhaa nchini Uingereza.

Alhamisi jioni mchumba wake Kajala Masanja alipakia video fupi iliyoonyesha wakikumbatiana baada yake kufika nyumbani.

"Amerudi 🥂💃❤" muigizaji huyo aliandika chini ya video ambayo alichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Mama huyo wa binti mmoja alionekana mwenye bashasha tele wakati alipokuwa akimlaki mchumba wake nyumbani.

Harmonize pia alichapisha video hiyo kwenye ukurasa wake na kutuma ujumbe kwa waliotabiri mabaya kwenye mahusiano yao.

"Loo hebu tazama jicho la mtabiri feki lilivyomtokaa😅, hebu  mtumie tena," aliandika.

Haya yanajiri huku kukiwa na tetesi zinazoendelea kwamba huenda hali sio nzuri katika mahusiano ya wasanii hao wawili.

Tetesi hizo zilianza siku kadhaa baada ya wawili hao kuchapisha jumbe za kutia wasiwasi kwenye kurasa zao.

"Niache peke yangu!" Kajala aliandika kwenye Instastori zake juzi.

Alifuatisha ujumbe wake na kauli zilizosema, "Niko katika hatua ya maisha yangu ambapo nahitaji amani na utulivu, sio mitazamo na mabishano... Kila kitu tunachopitia maishani ni mtihani wa kupiga hatua inayofuata au kukaa katika sehemu moja."

Harmonize kwa upande wako alionyesha kuchokeshwa na jambo ambalo hakubainisha na kutaka aachwe peke yake pia. 

“Usijivunie mwanadamu hata siku moja, ata akwambie anakupenda vipi. Katika maisha haya nadhani, unamhitaji Mungu tu. Mwanadamu, Ipo siku atakuvunja moyo. Ndio, niache pia. Sihitaji mtu yeyote," alisema.

Katika chapisho lingine, bosi huyo wa Kondegang alibainisha kuwa hataki matatizo na mtu yeyote ila anataka tu kufanya muziki na kulinda familia yake.

"Kama kuna unayemjua ana mchango mkubwa kwenye maisha yangu kumpita Mungu Baba basi ana haki ya kuongea lolote!! Nami nitamuachia yeye amjibu Inshallah" alisema.

Haya yanajiri huku mke wa zamani wa mwimbaji huyo, Sarah Michelloti akidaiwa kuwasilisha kesi ili kuomba mahakama kumshinikiza wagawane mali.

Sarah na Harmonize walikuwa kwenye mahusiano ya muda mrefu kabla ya msanii huyo kukutana na Kajala.

Kajala na Harmonize walirudiana mapema mwaka huu baada ya kutokuwa na maelewanao kwa kipindi cha takriban mwaka mmoja.

Walikuwa wametengana Aprili mwaka jana kufuatia madai kwamba Harmonize alijaribu kumtongoza bintiye Kajala, Paula.