Rotimi hatimaye afunguka sababu ya kuchumbiana na Vanessa Mdee

Muigizaji huyo alisema kando na Vanessa kuwa mrembo, pia anajua jinsi na wakati wa kuwa shupavu.

Muhtasari

•Rotimi anachumbiana na mwimbaji wa Tanzania Vanessa Mdee na wako na mtoto mmoja wa kiume pamoja.

•Rotimi aliwataja wanawake wa Kiafrika kuwa wanyenyekevu.

Vanessa Mdee na Rotimi
Image: INSTAGRAM

Muigizaji wa Nigeria anayeishi Marekani Olurotimi Akinosho almaarufu Rotimi ameeleza kwanini yuko kwenye mahusiano na mwanamke wa Kiafrika.

Rotimi anachumbiana na mwimbaji wa Tanzania Vanessa Mdee na wako na mtoto mmoja wa kiume pamoja.

Akizungumza katika mahojiano na The Pivot Podcast, Rotimi aliwataja wanawake wa Kiafrika kuwa wanyenyekevu.

"Unapokuwa na mwanamke wa Kiafrika, unapata mwanamke ambaye ni makini kuhusu tunavyoelewa jinsi ya kumtendea mwanaume na jinsi ya kunyenyekea," alisema.

Rotimi alisema kando na Vanessa kuwa mrembo, pia anajua jinsi na wakati wa kuwa shupavu.

"Ni usawa tu ambao ni vigumu kuupata na sisemi kuwa haupati hivyo kwa wanawake wa Marekani, lakini wanawake wengi wa Kiafrika wamefanywa kuwa malkia katika akili zao na pia kuwa wake wazuri."

Mnamo Septemba 28, wanandoa hao walisherehekea siku ya kuzaliwa ya mtoto wao Seven.

Vanessa alimmwagia sifa kochokocho mwanawe huku akimshukuru Mungu kwa kumjalia mtoto wa kiume.

"Mtoto wangu, wewe ni zawadi ya kimungu na ninaheshimiwa kuwa Mama yako. Asante kwa kuwa baraka yetu kuu," aliandika.

Rotimi pia alimtaja mkewe kama mwanamke mwenye nguvu.

Wanandoa hao wanadaiwa kupanga kufanya harusi ya Kizungu.