"Yeye ndiye alinitongoza!" Aliyekuwa mume wa dadake Diamond azungumzia ndoa yao ya miezi 3

Msizwa alisisitiza kwamba yeye sio sababu ya kutengana kwao

Muhtasari

•Bw Msizwa amepuuzilia mbali madai kwamba alitumia uchawi kumtongoza aliyekuwa mke wake, Esma Platnumz..

•Pia alikana kuwa ndoa yake na Esma ilikuwa ni biashara tu na kusisitiza kuwa walikuwa wameoana kwa kweli.

Mfanyibiashara Yahya Msizwa na dadake Diamond, Esma Platnumz.
Image: HISANI

Mfanyibiashara maarufu wa Bongo Yahya Msizwa amepuuzilia mbali madai kwamba alitumia uchawi kumtongoza aliyekuwa mke wake, Esma Platnumz..

Wawili hao walifunga pingu za maisha mwaka wa 2020 ila zikawashikilia kipindi kifupi kwani hatimaye waliachana baada ya miezi mitatu tu.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa hoteli yake, Bw Msizwa alidai kuwa dada huyo wa Diamond ndiye aliyemtongoza.

"Mimi ndiye nilitongozwa. Sio mimi nilienda kumtongoza yeye. Hiyo kabisa nakwambia. Aliniambia anataka nimuone ili nimsitiri,"  alisema.

Pia alitupilia mbali madai kuwa ndoa yake na Esma ilikuwa ni biashara tu na kusisitiza kuwa walikuwa wameoana kwa kweli.

"Tulioana kwa kweli lakini ikatokea sintofahamu ikawa hivo na huwezi kulazimisha kitu ambacho kimetokea," alisema.

Mfanyibishara huyo alisisitiza kwamba yeye sio sababu ya kutengana kwao. Alibainisha kuwa ana wake wengine wawili ambao wamekaa naye kwa miaka mingi tofauti na Esma ambaye alikaa kwa muda mfupi sana

"Mimi sipendi matatizo. Umri niliofikia sijawahi kukaribisha matatizo. Kama Mtu alikuja akaondoka yeye ndiye mwenye matatizo, sio mimi," alisema.

Msizwa na Esma walifunga ndoa mnamo Julai 30, 2020 ila wakatengana na kuenda njia tofauti miezi mitatu baadae.

Takriban miezi miwili iliyopita Esma alipuuzilia mbali madai kuwa shida  yake ya kukosa kutulia kwenye ndoa moja  kwa muda mrefu hutokana na ustaa unaomuingia kwa kuwa dada mkubwa wa mwanamuziki Diamond Platnumz.

Katika mahojiano na Wasafi Media, Esma alidai kwamba kamwe hajawahi kujipiga kifua kuhusu uhusiano wake na bosi huyo wa WCB.

"Sijawahi kusema eti kujigamba mimi ni dadake fulani. Nikiwa na mtu mwingine siwezi kusema eti mimi ni dadake fulani,"

Alieleza kwamba sababu kuu inayochangia kusambaratika kwa mahusiano yake ni ukosefu wa maelewano kati yake na mwenzie.

"Mimi sijimwambafai eti kwa sababu mimi ni dadake fulani. Mimi ninajiamini na ninajikubali kwa sababu mimi ni mwanamke anayetafuta mwenyewe. Najua kutafuta pesa , najua kujilipia kodi , najua kujijengea, najua kulisha watoto  wangu. Pia nina wafanyikazi nyumbani, ninasomesha watoto wangu kwa gharamu. Kwa hiyo mwanaume hawezi kunibabaisha , ndugu yangu nikiona hatuelewani basi shika huko nami nishike huku. Maisha mafupi na nishateswa huko sana," Alisema.

Aidha aliweka wazi kwamba kamwe hajawahi kujinufaisha  kwa umaarufu wa kaka yake wala kutegemea mali yake.