Fahamu sababu kuu kwa nini Diamond hatafunga ndoa hivi karibuni

Staa huyo wa Bongo hajaonyesha dalili ya kuoa hivi karibuni.

Muhtasari

•Mtangazaji Idriss Kitaa alifichua kuwa Diamond anahofia kujitosa kwenye ndoa kwa kuwa hatua hiyo inaweza ikampunguzia mashabiki.

•Idriss alisema Diamond anaruhusiwa kuwa na wapenzi zaidi ya mmoja kama ilivyodokezwa awali na  mwandani wake Haji Manara.

katika ziara yao ya Ufaransa.
Diamond Platnumza na anayedaiwa kuwa mpenziwe, Zuchu katika ziara yao ya Ufaransa.
Image: INSTAGRAM// ZUCHU

Staa wa Bongo Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz hatajitosa kwenye ndoa hivi karibuni, Mtangazaji wa Wasafi Media Idriss wa Kitaa amefichua.

Katika mahojiano na Mbengo TV, Idriss aliweka wazi kuwa bosi wake hajaonyesha dalili zozote za kufunga pingu za  maisha hivi karibuni.

"Ninachokijua Diamond sio wa kuoa leo wala kesho. Hata haonyeshi dalili za kuoa kwa kweli," Idriss alisema.

Mtangazaji huyo wa kipindi cha Mashamsham alifichua kuwa kazi za Diamond ndizo zinamzuia kuwa na mke na kuanzisha familia.

Alisema kuwa bosi huyo wa WCB anahofia kujitosa kwenye ndoa kwa kuwa hatua hiyo inaweza ikampunguzia mashabiki hasa wa kike.

"Sasa hivi kuna mwanamke ana ndoto ya kuwa na Diamond. Anajua ipo siku atampata. Kazi yake ni muziki, hii kazi ni ya kiufundi sana, akioa sasa hivi atapunguza mashabiki," alisema.

Aliongeza, "Kuna mwanamke huko nje anaamini ipo siku atakutana na Diamond na atakuwa mpenzi wake. Akioa atakuwa amemkatisha mwanamke huyo tamaa na ataondoka kwenye mapenzi na ushabiki shughuli inakuwa imekwisha."

Idriss hata hivyo alibainisha kuwa staa huyo wa Bongo anaruhusiwa kuwa na wapenzi zaidi ya mmoja kama ilivyodokezwa awali na msemaji wa Yanga SC na ambaye ni mwandani wake, Haji Manara.

Haya yanajiri takriban miezi mitatu baada ya Diamond mwenyewe kuweka wazi kuwa hana mpango wa kuoa na kutulia kwenye ndoa muda wowote hivi karibuni.

Katika mahojiano na DW Africa, mwimbaji huyo aliulizwa ni lini anapanga kutulia kwenye ndoa ikizingatiwa kwamba umri wake unazidi kusonga kwa kasi.

“Unapanga lini kutulia lini, yaani lini unaoa mwanamke?” aliulizwa.

Huku akitoa jibu lake, Diamond alisema kuwa kwa sasa anataka kuzingatia taaluma yake ya usanii na kueleza hofu yake kuwa pindi akijitosa kwa ndoa, basi azma yake ya kufanya muziki zaidi itakuwa imevurugika.

“Una maanisha nini, mimi tayari nimeshatulia. Lakini hiyo unajua mimi bado nataka kuwapa muziki kwa sana, mimi chenye nimeona ni kwamba nikioa mwanamke basi atanitoa kwenye njia yangu ya kufanya muziki na kuvuruga azma yangu ya kufanya muziki zaidi, nimeliona hilo kutoka kwa rafiki zangu wote. Kwa sasa wacha niwape muziki na ikifika muda nimekaribia kustaafu basi nitaoa,” Diamond alisema.

Alipoulizwa wakati maalum atakapooa, msanii huyo alionekana kukwepa swali hilo kabisa na kusema kwamba muda wowote tu hivi karibuni chochote kinawezekana na kusisitiza kwamba  Mungu ndiye mpangaji wa vyote.

Diamond hata hivyo amekuwa akidaiwa kuwa kwenye mahusiano na msanii wake Zuchu ila bado hawajawahi kufichua mipango yao.