Zuchu ashindwa kuzuia hasira baada ya nyimbo zake kukejeliwa

Mwimbaji huyo amekuwa akizipigia debe nyimbo zake mbili mpya 'Kwikwi' na 'Love.'

Muhtasari

•Zuchu amekuwa akizitangaza ngoma hizo haswa kwenye Instagram tangu alipoziachia siku kadhaa zilizopita.

•Shabiki aliyeonekana kumfika kwenye koo ni ambaye alidai kuwa anazitangaza ngoma hizo kwa kuwa ni mbaya.

Image: INSTAGRAM// ZUCHU

Malkia wa Bongo Zuhura Othman almaarufu Zuchu ameendelea kuzipigia debe nyimbo zake mbili mpya 'Kwikwi' na 'Love.'

Msanii huyo wa WCB amekuwa akizitangaza ngoma hizo haswa kwenye Instagram tangu alipoziachia siku kadhaa zilizopita.

Baadhi ya mashabiki wake wamekuwa wakijirekodi wakishiriki mashindano ya densi ya nyimbo hizo zake kisha kumtumia. Baada ya kuzipokea amekuwa akizichapishwa kwenye ukurasa wake kama njia mojawapo ya kuzipigia debe.

"Endeleeni kufurahia video za densi," alisema katika chapisho lake la hivi punde.

Wanamitandao wengi wamezipokea nyimbo hizo vyema na kama kawaida hakukosi wakosoaji katika kila jambo.

Baadhi ya wanamitandao wamemshtumu binti huyo wa Khadija Kopa kwa kuwalazimisha kuzikubali nyimbo zake. Wengine wamekuwa wakimkejeli hasa kwa wimbo Kwikwi wakidai kuwa haupendezi.

"Napenda nyimbo zako sanaaa, lakini kwa hii kwikwikwi , inaudhi kusema kweli. Namaanisha ngoma ni mbaya nisiwe muongo. Usitoe hata video yake toa hit song ingine," mtumizi wa Instagram mmoja alimwambia.

Zuchu alijibu kwa kejeli, "Sawa, nimekusikia mkuu."

Shabiki aliyeonekana kumfika kwenye koo ni ambaye alidai kuwa anazitangaza ngoma hizo kwa kuwa ni mbaya.

"Hizi nyimbo mbili alizotoa mbovu mno ndio maana anazifanyia promo," shabiki aliandika chini ya chapisho la Instagram.

Staa huyo kutoka Zanzibar alijibu kwa kusema, "Na kuna mzazi wako huko anafurahi kuwa ana binti mwenye akili timamu😂 Kwa hiyo tutoe kimya kimya da Monica."

Kufikia wakati wa kuchapisha makala haya, wimbo 'Kwikwi' ulikuwa umetazamwa zaidi ya mara 668,000 kwenye mtandao wa  YouTube ilhali 'Love' ulikuwa na umefikia watazamaji zaidi ya milioni moja.