(+video) Ajuza, 61, aliyempigiia Ruto kampeni asema anataka mume, "damu yangu ni moto"

Wazee huanzia kutoka miaka 70 na kwa kuwa mimi bado sijafika hapo, bado ninajihisi mbichi - Waihera alipinga kuitwa mzee.

Muhtasari

• Alisema alikuwa katika ndoa kwa miaka kumi kabla ya aliyekuwa mumewe kumtoroka na kumfuata msichana mdogo.

Msimu wa kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9 uliokamilika taktribani miezi miwili iliyopita, kulikuwepo na ajuza mmoja aliyejitokeza wazi na kumuidhinisha rais wa sasa William Ruto kipindi hicho akiwa kama naibu rais na mgombea urais.

Mama huyo aliyefahamika kwa jina Pauline Waithera kwa mara nyingine tena amerejea kwenye vyombo vya habari baada ya kufanya gumzo katika runinga ya NTV na wanahabari Fridah Mwaka na Lofty Matambo.

Katika mahojiano hayo ambayo yalichukua dakika 20 na ushee, mama Waithera mwenye umri wa miaka 61 alieleza kwamba ako sokoni na anatafuta mwanaume wa kumuoa kwa kile alisema damu yake bado ni moto sana.

Waithera alisema kwamba hii haitakuwa mara ya kwanza anajaribu bahati kwenye ndoa kwani aliwahi kuwa katika ndoa kwa takribani miaka 10 kabla ya mumewe kipindi hicho kumtema na kuendea vidosho waliokuwa wanavalia kwa njia ya kuvutia.

“Tulioana kutoka mwaka 1973 hadi 1983, na ningemtunza. Hata hivyo, alikutana na wanawake vijana waliovalia mavazi yasiyopendeza na kunikimbia,” Waithera alieleza.

Alionekana kuwalaumu wanaume kuwa hawatosheki na kusema kwamba licha ya kujitoa kwa hali na mali kwa aliyekuwa mumewe huyo, bado hakutosheka na mwisho wa siku alimkimbia kutafuta makazi kwa vidosho wabichi.Ajuza huyo alisema hata hivyo mumewe huyo alifariki mwaka 2014 hata kama hawakuwahi rudiana tangu kuachana mwaka 1983.

“Wanaume hawaridhiki hata kama unajitoa vipi kwao. Huyo aliyekuwa mume wangu kabla ya kunitoroka alifariki mwaka wa 2014, lakini hatukuwa tumerudiana kabisa,” mama Waithera alibainisha.

Licha ya kuwa na umri mkubwa wa miaka zaidi ya sitini, Waitherqa alionekana kutofurahishwa na watu wanaomwita ajuza na kueleza kwamba kwa anavyojua yeye, wazee huanzia miaka 70 kuendelea mbele.

Kwa utani, mama Waithera alisema kuwa anataka mume kwa sababu damu yake ni moto kutokana na kula vyakula moto pia.

“Sasa nimerudi sokoni kwa sababu ninajihisi mdogo. Sipendi kuitwa mzee, Wazee huanzia kutoka miaka 70 na kwa kuwa mimi bado sijafika hapo, bado ninajihisi mbichi. Unapokula chakula cha moto, pia unahisi joto," ajuza huyo alisema huku wanahabari hao wakiangua kicheko.