"Ni wa Diamond!" Vera ajibu baada ya kuulizwa ikiwa Otile Brown ndiye baba wa bintiye

Mwanasoshalaiti huyo ameweka wazi kuwa yuko kwenye ndoa rasmi na Brown Mauzo.

Muhtasari

•Mtumizi wa Instagram alitaka kujua ikiwa mpenzi wake wa zamani, Otile Brown, ndiye baba mzazi wa binti yake wa mwaka mmoja, Asia Brown.

•Mama huyo wa binti mmoja pia aliweka wazi kuwa kamwe hawezi kubali kuwa mke mwenza katika ndoa yoyote.

Image: INSTAGRAM// VERA SIDIKA

Mwanasoshalaiti Vera Sidika ameendelea kuwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha Maswali na Majibu (Q&A) kwenye Instagram.

Wanamitandao wameendelea kumuuliza maswali, kutoa maoni na hata kumwandikia jumbe za pongezi ambazo amekuwa akijibu. Yawe maswali/maoni chanya au hasi, mwanasoshalaiti huyo amekuwa akiyajibu.

Katika moja ya maswali, mtumizi mmoja wa Instagram alitaka kujua ikiwa mpenzi wake wa zamani, Otile Brown, ndiye baba mzazi wa binti yake wa mwaka mmoja, Asia Brown.

"Je, Otile ndiye baba mzazi wa Asia," shabiki aliuliza.

Kwa utani Vera alijibu, "Lmaooo. Hapana. Diamond Platnumz ndiye😂😂😂,"

Mwanasoshalaiti huyo mwenye umri wa miaka 33 alijifungua mtoto wake wa kwanza mnamo Oktoba 20, 2022.

Hii ilikuwa takriban mwaka mmoja baada ya kujitosa kwenye mahusiano na mwimbaji Brown Mauzo. Baada ya kuishi pamoja kwa miezi kadhaa, mwanasosholaiti alipachikwa ujauzito Februari mwaka jana.

Vera Sidika na Otile Brown walitengana katika njia tatanishi mwezi Agosti 2018 baada ya kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi kwa miezi michache. Baada ya kutengana kwao, wasanii hao wawili walinyoosheana vidole vya lawama huku kila mmoja akiibua madai mazito dhidi ya mwenzake.

Kufuatia kuvunjika kwa mahusiano hayo, Otile alikutana na kipusa mrembo kutoka Ethiopia, Nabayet na kuchumbiana kwa takriban miaka minne kabla ya wao kutengana mapema mwaka huu.

Vera alikutana na Brown Mauzo Agosti 2020 na kuanza kuishi pamoja katika mpango wa kujenga familia pamoja.

Katika kipindi cha Q&A anachoendeleza, Vera amefichua kuwa yuko kwenye ndoa rasmi na Brown Mauzo.

"Ndio. Tuko na vyeti wa ndoa. Ni sherehe ya harusi tu hatujafanya," alimjibu shabiki aliyetaka kujua ikiwa ndoa yao ni rasmi.

Mama huyo wa binti mmoja pia aliweka wazi kuwa kamwe hawezi kubali kuwa mke mwenza katika ndoa yoyote.

"Kila mtu yuko na maoni yake lakini kwangu binafsi siwezi kuwa mke wa pili. Ata iwe Bill Gates. Ni heri nikae single," alisema.

Pia alibainisha kuwa hawezi kuchumbiana na mwanaume ambaye anapenda kandanda kupindukia.