Zuchu kupeperusha bendera ya Afrika Mashariki katika tuzo za kifahari za kimataifa

Msanii huyo wa WCB ameteuliwa katika Tuzo za MTV EMA 2022, kipengele cha Best African Act.

Muhtasari

•Zuchu atamenyana na wababe wengine wa muziki kutoka Afrika kama vile Arya Starr, Burna Boy, Black Sheriff, Tems na Musa Keys.

•Mwaka wa 2021 Diamond Platnumz aliteuliwa katika tuzo hizo lakini hakufanikiwa kutwaa ushindi. 

ZUCHU NA DIAMOND PLATNUMZ
Image: WASAFI/INSTAGRAM

Staa wa Bongo Zuhura Othman Soud almaarufu Zuchu ameendelea kuthibitisha ubabe wake katika muziki na kujibainisha kuwa malkia wa muziki wa Bongo huku akiteuliwa kwa tuzo ya kifahari ya kimataifa.

Msanii huyo wa WCB ameteuliwa  katika Tuzo za MTV EMA 2022, kipengele cha Best African Act. Atamenyana na wababe wengine wa muziki kutoka Afrika kama vile Arya Starr, Burna Boy, Black Sheriff, Tems na Musa Keys.

Uteuzi huo umemfanya kuwa Zuchu kuwa msanii wa kwanza kabisa wa kike kutoka ukanda wa Afrika Mashariki kuteuliwa katika tuzo hizo za kifahari zinazofanyika kila mwaka. Hata hivyo, kuna wasanii wengine kadhaa kutoka Bongo ambao wamewahi kupata uteuzi kama huo katika miaka ya hapo awali.

Mwaka wa 2021 Diamond Platnumz aliteuliwa katika tuzo hizo lakini hakufanikiwa kutwaa ushindi. Hapo awali, mwaka wa 2015, alishinda tuzo hizo katika vipengele vya Best African Act na India Act.

Staa mwingine wa Bongo, Alikiba, alishinda tuzo ya MTV EMA 2016 katika kipengele cha msanii bora wa Kiafrika.

Zuchu ambaye amekuwa akiachia kibao baada ya kibao tangu kujiunga na WCB mwaka wa 2020 sasa anakuwa msanii wa tatu kutoka Tanzania kuwahi kuteuliwa katika tuzo hizo. Ikiwa atafanikiwa kupata ushindi atakuwa mshindi wa tatu kutoka Tanzania na kwanza wa kike kutoka Afrika Mashariki.

Mzaliwa huyo wa Zanzibar ni binti wa gwiji wa taarab Khadija Kopa na ndugu zake pia ni wasanii. Kakake, marehemu Omar Kopa alikuwa msanii tajika huko Bongo kabla ya kuaga dunia mwaka wa 2007 na ndugu zake wengine Suma Kopa na Black Kopa pia wamejikakamua kuliendeleza jina la familia katika usanii.