"Nitamuoaje?" Diamond akanusha waziwazi mahusiano ya kimapenzi na Zuchu

"Sasa nitamuoaje wakati ni msanii wangu Boss?" alihoji.

Muhtasari

•Diamond amekana wazi uhusiano wa kimapenzi na mtunzi huyo wa kibao 'Sukari' na kusisitiza kuwa ni msanii wake tu.

•Katika jibu lake, pia alifafanua kuhusu busu  aliloonekana akimpa Zuchu kwenye video hiyo ambayo amefuta tayari.

ZUCHU NA DIAMOND PLATNUMZ
Image: WASAFI/INSTAGRAM

Staa wa Bongo Diamond Platnumz kwa mara nyingine ameweka wazi kuwa uhusiano wake na Zuchu ni wa kikazi tu.

Diamond amekana wazi uhusiano wa kimapenzi na mtunzi huyo wa kibao 'Sukari' na kusisitiza kuwa ni msanii wake tu.

Alilazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya mmoja wa mameneja wake , Hamisi Shaban Taletale almaarufu Babu Tale, kumpa shinikizo kubwa  la kumuoa binti huyo wa gwiji wa muziki wa taarab ,Khadija Kopa.

"Fanya basi uoe unanichelewesha ujue," Tale alimwambia bosi huyo wa WCB chini ya video aliyopakia kwenye Instagram ikimuonyesha Zuchu akimkabidhi mkufu ghali wa dhahabu kama zawadi ya siku ya kuzaliwa.

Diamond ambaye alionekana kutofurahishwa na ujumbe huo wa meneja wake alihoji jinsi angeweza kumuoa msanii wake.

"Sasa nitamuoaje wakati ni msanii wangu Boss?" alihoji. 

Katika jibu lake, pia alifafanua kuhusu busu  aliloonekana akimpa Zuchu kwenye video hiyo ambayo amefuta tayari.

"Hilo busu hapo lisiwatishe viongozi.. ni Salaam za Kijerumani hizo," alisema.

Jumatano, Diamond alionyesha mkufu wa thamani ambao alipewa na Zuchu kama zawadi ya siku ya kuzaliwa.

Chini ya video hiyo, Diamond alimshukuru msanii huyo wake kwa zawadi hiyo na kueleza jinsi anavyomthamini.

"Maneno hayawezi kuelezea shukran yangu kwa hili Zuuh.. nisije nikatereza kuandika waandishi wakapa kutoa stori bure, ila jua nakushukuru sana, na siku zote utaendelea kuwa pale," aliandika mwimbaji huyo.

Katika video hiyo fupi, mastaa hao wawili wa Bongo walionekana wakikumbatiana kwa furaha na hata kwa wakati mmoja kubusu midomoni.

Kabla ya kufutwa, wanamitandao walijumuika chini ya chapisho hilo na kuandika maoni mseto kutokana na maudhui ya video hiyo.