Mwanafunzi wa chuo kikuu auza figo yake ili kumnunulia mpenziwe Iphone 14

Simu ya Iphone 14 ilizinduliwa takribani mwezi mmoja uliopita na inauzwa kwa bei ya Ksh 299,000.

Muhtasari

• Iliarifiwa kwamba alimnunulia mpenzi wake simu ya gharama kwa sababu ya kiwango cha upendo wake kwake.

Image: Tweeter

Mapenzi ni kipofu. Mapenzi yanaweza kusababisha mtu akatekeleza kwenye maamuzi magumu pasi na kujua wala kujali matokeo yake mbeleni.

Taarifa za mwanafunzi mmoja wa chuo kikuu aliyesemekana kuuza figo yake moja kwa ajili ya kumnunulia mpenzi wake simu mpya aina ya Iphone 14 pro max zimewashangaza sana wanamitandao.

Habari hizo zilizochapishwa kwenye vyombo vingi vya habari nchini Nigeria zilieleza kwamba kijana huyo mwanafunzi wa chuo kikuu cha Port Harcourt alipita mipaka katika kuonesha mapenzi yake kwa mpenzi wake kwa kuiweka rehani figo yake moja ili kumnunulia zawadi ya simu kali.

Iliarifiwa kwamba alimnunulia mpenzi wake simu ya gharama kwa sababu ya kiwango cha upendo wake kwake.

Picha zinazozunguka kwenye mitandao ya kijamii zinamuonyesha akiwa ameshika iPhone huku akionyesha tumbo lake na plasta upande wa kulia wa karibu na mahali figo inakusudiwa kuwa.

Mtumiaji wa mitandao ya kijamii alipakia hadithi hiyo, akiandika;

”Mwanafunzi wa Uniport ametoka kuuza FIGO Ili kumnunulia Mpenzi wake IPHONE 14. Anasema pia anampenda msichana huyo”

Wanamitandao walishangazwa na kitendo hicho amabcho wengi walikifananisha na kujitoa kafara huku wengine pia wakisema ni kama kujitoa mhanga kwa ajili ya mapenzi.

“Wasiwasi wangu ni kama anaweza kuutumia vyema UWEKEZAJI huu wa maisha. Je, anajua jinsi ya Kurudisha uwekezaji huu?” mmoja aliuliza.

Simu hiyo ya Iphone 14 ilizinduliwa takribani mwezi mmoja uliopita na kampuni ya Apple na kwa bei ya wastani nchini Kenya inauzwa kwa takribani laki 2 na elfu tisini na tisa.