Akothee hatimaye afichua lugha yake ya mapenzi iliyomvutia kwa mpenziwe mzungu

Msanii huyo amethibitisha kuwa uchapakazi wa mpenziwe ndio uliomvutia kwake.

Muhtasari

•Katika ukurasa wake wa Instagram, alichapisha video iliyomwonyesha mpenzi huyo wake mzungu akiwa anafanya kazi mida ya majogoo.

•Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 42 pia alimhakikishia mpenziwe kuhusu mapenzi yake makubwa kwake.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji na mjasiriamali Esther Akoth almaarufu Akothee ameweka wazi kinachomvutia zaidi kinachomvutia zaidi katika masuala ya mapenzi. 

Kwa mara nyingine msanii huyo amethibitisha kuwa uchapakazi wa mpenzi wake mpya ndio uliomvutia ajitose kwenye mahusiano naye.

Katika ukurasa wake wa Instagram, alichapisha video iliyomwonyesha mpenzi huyo wake mzungu akiwa anafanya kazi mida ya majogoo.

"Omosh wangu, mwendo wa saa kumi na moja  asubuhi, sasa mnajua lugha yangu ya mapenzi," aliandika chini ya video hiyo.

Jumapili, mama huyo wa watoto watano aliweka wazi kuwa mapenzi anayopata sasa kutoka kwa mzungu huyo ambaye amebatiza jina la Omosh ni mapenzi ambayo hajawahi kushuhudia hapo awali.

Alibainisha kuwa anafurahia sana na ameridhika  katika mahusiano yake mapya.

"Maisha niliyoyasubiri tangu miaka 40.. Mungu amenijaalia  mtu tunayelingana, kila kitu changu kwenye picha moja, ikibidi nife leo, sasa naweza kukiri kuwa nakufa kwa furaha," alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 42 pia alimhakikishia mpenziwe kuhusu mapenzi yake makubwa kwake.

Siku kadhaa zilizopita Akothee alidokeza kuwa bidii kubwa ya mpenzi huyo wake mwenye umri wa makamo ndiyo iliyomvutia kwake.

Kwenye Instagram, alipakia picha iliyomuonyesha akiwa na mpenzi wake wakitembelea shamba lake. Wawili hao walionekana wakizunguka shamba hilo kubwa na kuzungumza na wafanyakazi waliokuwa pale.

"Habari za asubuhi wafalme na malkia. Mnaona sababu kwa nini Bwana Omondi aliuteka moyo wangu. Huwa ameamka kabla ya saa kumi na moja asubuhi, aah Mungu huyu💪💪💪💪.. na ndio maana nilimpatia jina Omondi," alisema.

Wakati huo mama huyo wa watoto watano pia alidokeza kwamba mpenzi wake mpya ni tajiri mkubwa.

Aidha alijigamba kuwa mahusiano yake mapya yamefanya akawa mwenye furaha zaidi na kuongeza urembo wake.

"Lakini huyu mzungu wangu amefanya nimekuwa mrembo na mwenye furaha sana, haki pesa wewe ni sabuni ya mapenzi. Hakuna kitu tamu kama kuchumbiana na mwanaume ako na pesa zake. Tamuuuu," alisema.

Akothee alitangaza mahusiano yake mapya mwezi uliopita baada ya kumficha mpenziwe hadharani kwa muda mrefu.

Haya yalitokea miezi kadhaa baada ya kuvunjika kwa mahusiano yake ya awali na aliyekuwa meneja wake Nelly Oaks.