Jackie Matubia na Blessing Lungaho wafunga harusi?

Mwigizaji huyo alipakia picha akiwa amevaa gauni ya harusi

Muhtasari

• Matubia alimshukuru Mungu kwa hatua hiyo kubwa ya maisha yake kwenye picha aliyopakia katika ukurasa wake wa Instagram.

Jackie Matubia

Mwigizaji Jackie Matubia aligeuka gumzo baada ya kudokeza kufunga pingu za maisha  leo Jumatatu.

Watumizi wa mitandao walibaki wakijiuliza maswali na kuwa na fikira za iwapo yeye na mpenzi wake Blessing Lungaho walikula yamini.

Matubia alizua gumzo hilo baada ya kupakia picha katika ukurasa wake wa Instagram akiwa amevalia gauni ya harusi.

Katika picha hiyo aliyopakia, Matubia alikuwa amevalia gauni hilo na kupambwa kwa kupodolewa kisha kuvalishwa taji la bibi harusi.

Alikuwa amehanikiza katika janibu zote kama mwanga wa mwezi na alikuwa ameshikilia koja la maua kisha akadokeza jinsi siku hiyo ilivyokuwa muhimu katika maisha yake.

"Hii siku imebarikiwa. Nakushukuru Mungu kwa yote uliyotenda na kwa yote utakayotenda, waah," Matubia aliandika kwenye picha hiyo.

Hata hivyo, mwigizaji huyo bado hajazungumzia jambo hilo wala kuweka wazi iwapo ni kweli alikuwa amefanya harusi.

Mpenzi wake pia hajapakia picha yoyote wala kudokeza kufunga pingu za maisha naye.

Matubia na Lungaho wamekuwa wakichumbiana kwa muda sasa baada ya Lungaho kumposa Matubia mwezi wa Aprili.

Lungaho aliandika ujumbe katika ukurasa wake wa Instagram baada ya hatua hiyo kubwa:

"Siku zingine humfanya mvulana kuwa mwanaume na mwanume kuwa shujaa. Jana usiku ulikuwa usiku wa mwanaume huyu," Lungaho aliandika baada ya sherehe hiyo ya kumposa mchumba wake.

Matubia pia hakuchelewa kuwajulisha mashabiki wake na pia alichapisha ujumbe huku akipakia video ya yaliyotokea.

"Aliniposa nikakubali. Nina hamu ya kuwa nawe maishani mwangu, kwa furaha na kukupenda kila wakati," Matubia aliandika akiwafahamisha mashabiki wake.