Kwa wapenzi wa mitandao ya kijamii, bila shaka mtakuwa mmeiona picha ya mzee mmoja ambaye alisemekana kuwa raia wa Uganda.
Mzee huyo ambaye picha yake akionekana kutangaza katika hafla ambayo wengi waliamini ni mazishi akiwa ameshikilia karatasi nyingi kwa mkono mmoja huku mkono mwingine ameshika kipaza sauti, picha hiyo ilisambazwa sana na hata wengi kuitumia kama kichekesho – meme.
Kulingana na jarida la Daily Monitor nchini Uganda, liliripoti kuwa mzee huyo kwa jina Godfrey Jjemba Matte, amerudi katika shughuli zake za kilimo baada ya kuripotiwa "kutumiwa na kutupwa na wanasiasa na watu mashuhuri."
Mzee huyo mwenye umri wa miaka 69, alijikuta akitrend kwenye mtandao na hivyo kumfanya kuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii inayotumika sana huku picha na katuni zikichorwa kutokana na mtindo wake wa kipekee wa kusoma matangazo ya mazishi.
Pia alipokea ahadi kama redio ya jamii, pikipiki na miwani ya dirisha na milango, ambayo anasema haijawahi kutimizwa.
“Watu bado wananiita mtu mashuhuri lakini nimerejea kwenye kilimo kwa sababu baadhi ya watu walikuja hapa na kunitumia kwa maslahi yao binafsi kisha kunitelekeza. Kuna mchungaji mashuhuri anayeishi Kampala ambaye aliahidi kunipa viunzi vya madirisha na vioo kwa ajili ya nyumba yangu mpya lakini bado hajatimiza ahadi hiyo. Unaweza kuona jinsi mtu wanayemwita mtu mashuhuri anavyolala,” jarida hilo lilimnukuu mzee Jjemba aliyeonekana kuchanganyikiwa.
Jjemba aliyekasirishwa pia alifichua kwamba aliacha kutoa mahojiano "ya bure" kwa waandishi wa habari kwa sababu hapati chochote kutoka kwa mahojiano.
Baba huyo wa watoto 11 alisema baadhi ya mali za nyumbani alizochangiwa, runinga ya aina yake iliibiwa hivi majuzi na majambazi waliovamia nyumbani kwake usiku.